Wanazuoni wa Kifiqhi wanasema kuwa: mtu atakayeiharibu funga yake kwa makusudi, antakiwa ima amtowe huru mtumwa,[1] au afunge miezi miwili mfululizo, au awalishe mlo mmoja maskini sitini mpaka washibe, au ampe kila mmoja kati yao kiwango cha gramu 750 ya nafaka ambayo inatambulikana kuwa ni chakula ndani ya jamii anayoishi ndani yake, na iwapo yeye atakuwa hana uwezo wa kufanya moja kati ya hayo, basi awape maskini kiwango cha chakula ambacho ana uwezo nacho, na pia akiwa hana uwezo wa kufanya hilo, basi atubie kwa Mola wake. Lakini kwa kuihadhari adhabu ya Mola wake, anatakiwa wakati wowote ule atakapokuwa na uwezo wa kulitekeleza moja kati yale yaliyotajwa, basi alitekeleze. Kwani hapo ndipo mja huyo atapokuwa na utulivu wa moyo wake.[2] Katika suala la kuwalisha au kuwapa nafaka maskini, maulamaa wamependekeza zaidi chakula hicho kiwe ni ngano, au unga wa ngano au pia mikate itokanayo na ngano.
Ni jambo la wazi kuwa Mola amemuacha huru mja wake katika kuchagua moja kati hayo yaliyotajwa hapo juu, na si lazima mtu kujifunga na moja ya hayo bila ya kuwa na uhuru wa kuchagua lile lililo rahisi kwake katika utekelezaji wa sheria ya Mola wake. Kwa hiyo mja atakuwa huru katika kufanya moja kati ya mambo yafuatayo:
1- afunge miezi miwili mfululizo.
2- awashibishe maskini sitini, au ampe kila mmoja wao kiwango cha gramu 750 ya nafaka, ambayo itakuwa ima ni ngano au unga wa ngano.
3- Ikiwa hawezi kutowa chakula, basi amuombe toba mola wake.
Lakini pia ni jambo lililotiliwa mkazo kufuata utaratibu uliotajwa hapo juu.[3]
Pia ni muhimu mtu kufahamu kuwa, iwapo yeye atakuwa ameiharibu funga yake kwa kupitia jambo la haramu, kama vile zinaa, au kula chakula cha wizi, au akawa amefanya mapenzi na mkewe huku akiwa katika hedhi, katika hali kama hiyo atatakiwa kuyafanya yote yaliyotajwa hapo juu, yaani yeye atatakiwa kulipa aina zote za fidia zilizotajwa hapo juu kwa pamoja.[4]
Pia iwapo mtu atakuwa hawatambui maskini ambao anatakiwa kuwalisha, basi anaweza kurejea kwenye ofisi za wanazuoni, ili aweze kuifikisha sadaka (fidia) yake, kwa ajili ya kupewa maskini wanaostahiki.
[1] Kuhusiana na kumtoa huru mtumwa, kwa kweli hilo ni suala ambalo haliwezekani kwa zama za leo, kwani zama za utumwa zimeshamalizika.
[2] Taudhihul-Masaail, cha Imam Khomeiny, juz/1, uk/931, suala la 1660 na 1661.
[3] Tahrirul-Wasila, cha Imam Khomeiny, juz/1, uk/289.
4 Taudhihul- Masail, cha Imam Khomeiny, juz/1, uk/931.