Please Wait
10632
- Shiriki
Rejeo mama na asili hasa zinazo aminika ambazo zimeyanukuu maandiko ya Sala na salamu (Ziara) za siku ya Ashura ni vitabu viwili, navyo ni: kitabu Kaamiluz-ziaaraat cha Jaa'far bin Muhammad bin Quulewaihi Qummiy, ambaye amefariki mwaka 348 Hijiria, na cha pili ni kitabu kiitwacho Misbaahul-mujtahid cha Sheikh Tusiy aliyezaliwa mwaka 385 na kufariki 460 Hijiria. Uchunguzi uliofanyika kuhusiana na mapokezi ya Riwaya iliyonukuliwa na Ibni Quulewaihi iliyoelezea Sala na salamu hizo, unaonesha kuwa Riwaya hiyo haina utata wala mashaka ndani yake, na huo ndio mtazamo wa wengi miongoni mwa wanazuoni wetu. Ama kuhusiana na mapokezi ya Riwaya yenye kuhusiana na Sala na salamu za siku ya Ashura yalionukuliwa kwenye kitabu Misbaahul-mujtahid yamegawika katika hali tatu tofauti, nazo ni kama ifuatavyo:
A: Baadhi ya wakati maandiko ya Riwaya hiyo yanaonekana kunukuliwa katika njia salama isiyo na utata, ambayo kitaalamu wapokezi wake huitwa (thiqatun), au kwa lugha yetu ya Kiswahili ni kwamba wapokezi wa Riwaya hiyo ni watu waaminifu, wakweli na wenye kuaminika kisawa sawa.
B: Baadhi ya wakati maandiko ya Riwaya hiyo yanaonekana kunukuliwa katika njia na mlolongo wa watu tofauti, miongoni mwao wakiwemo wale wapokezi wanaoaminika na kutegemewa, huku waliobakia wakiwa ni watu wasiotambulikana sifa zao kuwa: je nao ni wenye kutegemeka au si wenye kutegemeka?
C: Baadhi ya wakati maandiko ya Riwaya hiyo yanaonekana kunukuliwa katika njia na mlolongo wa watu tofauti, miongoni mwao wakiwemo wale wapokezi wanaoaminika na kutegemewa, vile vile wakiwemo wapokezi ambao habari zao hazitambulikani kisawasawa, lakini kwa kutokana na sababu pamoja na ishara maalumu zenye kuashiria kupatika kwa aina maalumu ya uaminifu juu ya wapokezi hao, hivyo basi nao pia wamekuwa ni miongoni mwa wapokezi wanaaminiwa kuwa ni waaminifu.
Kwa hiyo sisi hatuoni dalili ya kuzidhoofisha Riwaya za mapokezi hayo, na hukumu iliyo sawa ni ile isemayo kuwa: Riwaya za mapokezi hayo hazionekani kuwa na mashaka ndani yake. Mpaka hapa tumeona kuwa Riwaya na maandiko yalinukuliwa kuhusiana na Sala na salamu maalumu zisomwazo ndani ya siku ya Ashura, zimeegemea kwenye msingi madhubuti usio na utata mbele ya wanazuoni.
Riwaya iliyozinukuu Sala na salamu za siku ya Ashura, haikudadisiwa tu katika mapokezi yake, bali kuna watu mbali mbali wenye wasiwasi na ukweli wa mtririko na mfumo wa maneno yake yalivyo, wasiwasi huo umepatikana kwa kutokana na ibara maalumu zenye kuwalaani Banii Umyya zilizomo ndani ya maandiko yake. Lakini hilo lisikutatize sana kwani jawabu lake unaweza kulipata kwenye maswali na majibu tliyokwisha kuyatafiti na kuyapatia tiba madhubuti, kwa sababu tayari jawabu za suala hilo zimeshatolewa. Kwa ufahamu zaidi rejea ufafanuzi wa jawabu kamili juu ya suala lako hapa chini.
Sala na salamu (Ziara) maalumu zisomwazo ndani ya siku ya Ashura zimetufikia sisi kupitia Maimamu wawili, nao ni Imamu Baaqir na Saadiq (a.s), na hilo ndilo linaloweza kutupa sisi uhakika kamili wa usalama wa Riwaya zilizozinukuu Sala na salamu hizo, hapa la kuzingatiwa ni kwamba: sisi hatukubaliani na Riwaya zenye kupingana na mafunzo ya Qur-ani au kupingana na Hadithi zilizo sahihi. Ufafanuzi ufuatao utatufafanulia vya kutosha kuhusiana na ukweli wa Riwaya zinazozungumzia uhakika wa Sala na salamu hizo:
1: Egemeo na tegemeo la mapokezi linalotegemewa katika kuzinukuu Sala na salamu za siku ya Ashura:
Vitabu viwili vifuatavyo ndivyo msingi mkuu unaotegemewa na wale wenye kuzinukuu Riwaya zinazoelezea Sala na salamu hizo, navyo ni: Kaamiliz-ziaraat cha Jaa'far bin Muhammad Quulewaihi Qummiy aliyefariki mwaka 384 Hijiria, na Misbaahul-mujtahid cha Sheikh Tusiy aliyezaliwa mwaka 385 na kufariki mwaka 460 Hijiria, nasi hatuna budi kuzihakiki Riwaya za vitabu viwili hivyo kwa makini na uangalifu ili kuweza kuufikia ukweli wa mambo ulivyo, uhakiki kamili kuhusiana na Riwaya zilizokuja katika vitabu hivyo ni kama ifuatavyo:
A: Kitabu Kaamiluz-ziaraat cha Ibnu Quuliweihi
Ibnu Quuliweihi kuhusiana na thawabu za Sala na salamu za siku ya Ashura ameandika yafuatayo:
حَدَّثَنِی حَکِیمُ بْنُ دَاوُدَ بْنِ حَکِیمٍ وَ غَیرُهُ عَنْ مُحَمَّدِ بْنِ مُوسَى الْهَمْدَانِی عَنْ مُحَمَّدِ بْنِ خَالِدٍ الطَّیالِسِی عَنْ سَیفِ بْنِ عَمِیرَةَ وَ صَالِحِ بْنِ عُقْبَةَ جَمِیعاً عَنْ عَلْقَمَةَ بْنِ مُحَمَّدٍ الْحَضْرَمِی، وَ مُحَمَّدِ بْنِ إِسْمَاعِیلَ عَنْ صَالِحِ بْنِ عُقْبَةَ عَنْ مَالِکٍ الْجُهَنِی عَنْ أَبِی جَعْفَرٍ الْبَاقِرِ ع قَالَ مَنْ زَارَ الْحُسَینَ ع یوْمَ عَاشُورَاءَ مِنَ الْمُحَرَّمِ...".
Maana ya maneno hayo ni kwamba: "Nimehadithiwa na Hakim bin Daawud bin Hakim pia nimehadithiwa na weengine wasiokuwa yeye hadithi iliotoka kwa Muhammad bin Musa Al-Hamdaaniy, kutoka kwa Muhammad bin Khalid Al-Ttayaalisiy, kutoka kwa Seif bin Umeira na Saleh bin Uqba, kutoka kwa Al-qama bin Muhammad Al-Hadhramiy na Muhammad bin Ismail, kutoka kwa Saleh bin Uqba, kutoka kwa Maliki Al-Juhaniy, kutoka kwa Abi Jaa'far Al-Baaqir (a.s) kwamba Yeye (a.s) amesema: "Atakayemsalia na kumtakia amani Imamu Husein (a.s) siku ya Ashura ya mwezi wa Muharram… ", hou ni mlolongo wa wapokezi wa Riwaya hiyo.
Pia kwa mara nyengine akizungumzia ukweli wa Hadithi ya Sala na salamu za siku hiyo ya Ashura amenukuu Riwaya isemayo: Alqama bin Muhammad amesema: "mimi nilikwenda kwa Abu Jaa'far (a.s) nikamwambia: nifundishe dua ya kusoma pale nitakapokwenda kulizuru kaburi la Imamu Husein (a.s), kisha nifundishe dua nyengine ya kusoma popote pale natakapokuwepo ili niweze kumsalia na kumtakia yeye amani hali nikiwa mbali na kaburi lake". Imamu (a.s) akasema: "Ewe Alqama! Pale utapotaka kumsalia na kumtakia amani Imamu Husein (a.s), ambapo utakuwa tayari umesha sali rakaa mbili, basi msalie na umtakie amani kupitia Sala na salamu maalumu za siku ya Ashura iwapo wewe utakuwa katika siku za Ashura kwa kusema hivi: (amani iwe juu yako ewe mwana wa Mtume wa Mola, amani iwe juu yako ewe mteuliwa wa Mola na mwana wa mteuliwa wake, amani iwe juu yako ewe mwana wa Amiril-muuminiina na mwana wa bwana wa manaibu (makhalifa (maimamu)), amani iwe juu yako ewe mwana wa Fatima ambaye ni mtukufu wa wanawake wa ulumwengu mzima).[1]
Hapo basi tomeona kuwa Riwaya hii imenukuliwa moja kwa moja kutoka kwa Imamu (a.s) kupitia watu wawili muhimu nao ni: Alqama bin Muhammad Hadhramiy na Malik bin Aa'yuni Al-Juhaniy.
Uhakika hasa wa mapokezi ya Riwaya hii ni kwamba: Riwaya hii imepokewa kupitia njia tatu tofauti, nazo ni kama ifuatavyo:
Kwanza: kupitia Hakim bin Daawud bin Hakim na wengineo, kutoka kwa Muhammad bin Musa Al-Hamdaaniy, kutoka kwa Muhammad bin Khalid Al-Ttayaalisiy, kutoka kwa Seif bin Umeira, kutoka kwa Alqama bin Muhammad Al-Hadhramiy.
Pili: kupitia Hakiim bin Daawud bin Hakim na wengineo, kutoka kwa Muhammad bin Musa Al-Hamdaaniy, kutoka kwa Muhammad bin Khalid Al-Ttayaalisiy, kutoka kwa Saleh bin Uqba, kutoka kwa Alqama bin Muhammad Al-Hadhramiy.
Tatu: kupitia Muhammad bin Ismail, kutoka kwa Saleh bin Uqba, Kutoka kwa Malik Al-Juhaniy, kutoka kwa Abu Jaa'far Al-Baaqir (a.s).
Katika mlolongo wa wapokezi waliotajwa katika kipengele cha tatu, kunaweza kupatikana aina mbili za makadirio: kadirio la kwanza ni kwamba: inawezekana kuwa Ibnu Quulawaihi amezinukuu Sala na salamu za siku ya Ashura kutoka kwenye kitabu cha Muhammad bin Ismail, kama alivyonukuu Sheikh Tusiy, kwani Sheikh Tusiy naye amenukuu Riwaya ya Sala na salamu za Ashura kutoka kwenye kitabu hicho hicho cha Muhammad bin Ismail, na kama hali itakuwa ndiyo kama hiyo, basi Riwaya hiyo itakuwa ni sahihi, kwani mapolezi sahihi yatakuwa ni kuanzia mpokezi wa mwanzo hadi kufikia kwa Muhammad bin Ismail, kwani wapokezi wote waliotajwa katika mlolongo wa mapokezi ya Riwaya hiyo wanahadithia nukuu zao kutoka kwa Muhammad bin Ismail, kisha yeye Muhammad bin Ismail anahadithia kutoka kwa Saleh bin Uqba, na mpaka hapo sisi tutakuwa hatuna mashaka na Riwaya hiyo.
Kadirio la pili ni kuwa: nukuu za Muhammad bin Ismail zimeegemea kwenye nukuu za Muhammad bin Khalid Al-Ttayaalisy huku mtindo wa mapokezi hayo ukiwa ni kama ifuatavyo: kutoka kwa Hakim bin Daawud, kutoka kwa Muhammad bin Musa Al-Hamdaaniy, kutoka kwa Muhammad bin Khalid Al-Ttayaalisy, kutoka kwa Muhammad bin Ismail bin Bazii, kutoka kwa Saleh Uqba, kutoka kwa Malik Al-Juhaniy. Lakini kadirio hili la pili ni kadirio dhaifu, kwani kadirio madhubuti ni lile lioneshalo kuwa: kitabu cha Muhammad bin Ismail katika zama za zamani, kilikuwa ni kitabu maarufu, kwa hiyo kwa asilimia kubwa tunaweza kusema kuwa Sheikh Tusiy na Ibnu Quulewaihi wote wawili wameinukuu Riwaya hizo zenye kuzungumzia Sala na salamu za siku ya Ashura kutoka kwenye kitabu hicho.
Uhakiki wa tegemeo na egemeo la Riwaya ya Ibnu Quulewaihi
Ibnu Quulewaihi katika utangulizi wa kitabu chake anasema:
Mimi sina uwezo wa kuzitambua Riwaya zote zile za Ahlul-Bait zilizopokelewa kuhusiana na Sala na salamu maalumu za siku ya Ashura au pia zile zisisizohusiana na suala hilo, lakini Riwaya zote zile nilizozinukuu katika kitabu hichi, ni Riwaya nilizozipokea kutoka kwa watu waaminifu wenye kuaminika miongoni mwa wafuasi wetu, na wala mimi sikunukuu katika kitabu hichi Riwaya za watu wasiotambulika ambao hunukuu Riwaya kiholela kutoka kwa watu wasio maarufu ambao si mashuhuri katika uwanja wa elimu ya Hadithi.[2]
Sheikh Hurru Aa'milimiliy alipokuwa akizungumzia uwaminifu wa wapokezi mbali mbali walioinukuu Riwaya ya Sala na amani za siku ya Ashura, ambao ukweli na uaminifu wao umethibitishwa pia na Ali bin Ibrahim, yeye (Sheikh Hurru Aa'miliy) alisema kuwa wapokezi hao ni waaminifu kwa mtazamo wake yeye, kisha baada ya hapo akaendelea kwa kusema: "pia Jaa'far bin Muhammad bin Quulewaihi ameukubali uaminifu wa wapokezi wa Riwaya zilizomo ndani ya kitabu Kaamiluz-ziaaraat, naye anaamini kuwa wapokezi wa Riwaya za kitabu hicho ni wakweli, na ufafanuzi uoneshao umakini na uaminifu wa wapokezi hao uliotolewa mwanzoni mwa kitabu Kaamiluz-ziaraat, ni wenye kufikisha ujumbe wa uaminifu wa wapokezi hao kwa njia ilio wazi zaidi kuliko hata ule ufafanuzi uliotolewa na Ali bin Ibrahim."[3]
Lakini Tusiysahau kuwa baadhi ya wanazuoni wamesema kuwa: mpokezi anayeaminika katika mlolongo wa wale wapokezi walioinukuu Riwaya hiyo, ni yule tu ambaye Ibnu Quulewaihi amenukuu kutoka kwake moja kwa moja, yaani yule mtu wa mwanzo ambaye amemhadithia Ibnu Quulewaihi Riwaya hiyo miongoni mwa wale wapokezi waliotajwa ndani ya mlolongo wa wapokezi wa Riwaya hiyo.[4] Na miongoni mwa wanazuoni wenye kukubaliana na mtazamo huo ni marehemu Ayatu-Llahi Khui (r.a).[5] Ili basi tuutimize ipaswavyo uhakiki wetu huu, ni vizuri zaidi kuwachunguza wapokezi wa Riwaya hiyo, na uchunguzi huo ni kama ifuatavyo:
Hakim bin Daawud bin Hakim:
Ingawaje mpokezi huyu hakusifiwa kwa uaminifu ndani ya vitabu vyenye kuchunguza maisha ya wapokezi wa Hadithi, lakini pia hakukuonekana kuwepo kitabu kilichomsifu yeye kwa udhaifu fulani. Jengine ni kwamba kuna waandishi walionukuu Hadithi mbali mbali kutoka kwake, na miongoni mwa walionukuu Hadithi kutoka kwa mpokezi huyu, ni mwandishi wa kitabu kijulikanacho kwa jina la Tahdhibu.[6] Muhammad Ruriy amemzungumzia mpokezi huyu na kumuhesabu kuwa ni miongoni mwa mashekhe[7] wa Ibnu Quulewaihi.[8] Maelezo hayo kuhusiana na mpokezi huyu, ni ujumbe tosha utufanyao sisi tumkubali yeye bila ya pingamizi yoyote.
Mummad bin Musa Al-Hamdani:
Kuna baadhi ya waandishi waliomshusha hadhi mpokezi huyu na kumdhoofisha,[9] lakini kama asemavyo marehemu Khui kuwa: kuteremshwa kwa hadhi ya mpokezi huyu, kunagongana na ile tathmini ya Ibnu Quulewaihi iliyompandisha daraja katika kitabu chake Kaamiliz-Ziaraat, kwa hiyo kuna mgongano unaopatikana katika jambo la yeye kuthaminiwa na Ibnu Quulewaihi na kwa upande wapili kutopewa hadhi na baadhi ya waandishi fulani, na kama hali itakuwa ndiyo hiyo, basi la msingi ni kuachana na kauli zote mbili, yaani ile kauli ya baadhi ya waandshi pamoja na ile ya Ibnu Quulewaihi, na hapo natija itakuwa ni kubakia mpokezi huyu katika giza la kutotambulikana uhakika wake.[10]
Kwanza Muhammad bin Khalid Al-Tayaalisiy na Muhammad bin Ismail bin Buzeigh tuwaweke kando, kwani tunakusudia kuwazungumzia watu hawa kwa marefu sana hapo baadae.
Uqba bin Qeis Kuufiy:
Yeye ni baba wa Saleh naye ni mfuasi wa Imamu Saadiq (a.s). kwa upande wake hakuna habari maalumu zenye kumtathmini yeye.[11]
Maalik Al-Juhaniy:
Njia ya pili ya mapokezi ya Hadithi tunayoitafiti katika uhakiki wetu huu, inatoka kwa Maaliki Al-Juhaniy, naye ameinukuu Hadithi hiyo moja kwa moja kutoka kwa Imamu (a.s), ambaye ametajwa kwa jina la Maaliki bin Aa'yuni Al-Juhaniy. Yeye ni miongoni mwa wafuasi wa Imamu Baaqiri (a.s), na Shekh Mufiid amesema kuwa Mpokezi huyu alikuwa akisifika kwa sifa njema mbele ya Imamu (a.s).[12] lilowazi ni kwamba, iwapo sisi tutakuwa hatuwezi kutoa hukumu ya moja kwa moja kuhusiana na usahihi wa Riwaya hii tunayoitafiti, basi pia hatuwezi kuitupa kando na kuihesabu kuwa ni miongoni mwa Hadithi dhaifu, kwani bado kuna baadhi ya njia maalumu zinazothibitisha usahihi wa Riwaya hii.
B- Kitabu Misbahul-Mujtahidi cha Sheikh Tusiy
Sheikh Tusiy naye ameinukuu Riwaya izungumziayo habari za Sala na salamu (Ziara) maalumu za siku ya Ashura katika kitabu tulichokitaja hapo juu, kupitia mifumo na milolongo miwili tofauti.
Mlolongo na mfumo wa kwaza
Yeye katika mfumo na mlolongo wake wa kwanza anasema hivi:
Imepokewa kutoka kwa Muhammad bin Ismail bin Buzeigh, kutoka kwa Saleh bin Uqba na Seif bin Umeira, kutoka kwa Alqama bin Muhammad Al-Hadhramiy amesema: (siku moja nilimuambia Abu Jaa'far: hebu nifundishe dua ya kumzuru Imamu Husein (a.s) katika siku ya Ashura pale nitakapokuwa karibu ya kaburi la Mtukufu Huyu, kisha pia nifundishe dua nyengine ya kusoma pale nitakapokuwa mbali na kaburi Lake (a.s) iwapo nitakuwa sina uwezo wa kumzuru Yeye katika kaburi Lake, labda pengine nikiwa niko mbali ya mji au hata nikiwa nyumbani kwangu pale nitakapotaka kumsalia na kumtakia amani. Imamu alijibu kwa kusema: kwanza Sali rakaa mbili, kisha msalimie na utoe takbira huku ukiwa umelielekea na kuliashiria kidole kaburi Lake (a.s), kisha soma Sala na salamu zifuatazo, kwani hizi ndizo Sala na salamu wanazozisoma Malaika pale wanapomsalia Yeye (a.s), na Sala na salamu hizo ni kama ifuatavyo: Amani iwe juu yako ewe Aba Abdi-Llahi… .[13] Kuna mambo muhimu ambayo ni lazima kuyatambua na kuyafanyia utafiti katika mtindo na mlolongo wa mapokezi yaliotajwa hapo juu, na ni muhimu katika kuuwivisha utafiti huo, kuyatambua mambo yafuatayo:
La kwanza: mlolongo wa wapokezi waliotajwa katika mapokezi haya umeishia kwa Muhammad bin Ismail Buzeigh.
Sheikh Tusiy Riwaya hii ameinuku kutoka katika kitabu cha Muhammad bin Ismail bin Buzeigh, na katika kitabu (Al-Fehrest) ameelezea namna ya yeye alivyo inukuu Riwaya hiyo kwa kusema: (Muhammad bin Ismail ana kitabu kinachozungumzia habari za Hija, na ndani yake kuna Riwaya iliyopokewa kwa mtindo ufuatao: tumepewa khabari kutoka kwa Ibnu Abi Jiid, kutoka kwa Muhammad bin Hassan bin Waliid, kutoka kwa Ali bin Ibrahim, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Muhammad bin Ismail, yaani Ibnu Abi Jiid kapokea kutoka kwa Muhammad bin Hassan bin Waliid, naye amepokea kutoka kwa Ali bin Ibrahim Qummiy, naye amepokea kutoka kwa baba yake, na baba yake naye amepokea kutoka kwa Muhaamad bin Ismail bin Buzeigh.[14]
Hivyo basi mlolongo sahihi wenye kuinukuu Riwaya hii kupitia kwa Sheikh Tusiy utakuwa ni kama ifuatavyo: kutoka kwa Sheikh Tusiy, kutoka kwa Ali bin Ahmad bin Muhammad bin Abi Jiid, kutoka kwa Muhammad bin Hassan bin Waliid, kutoka kwa Ali bin Ibrahim Qummiy, kutoka kwa Ibrahim, kutoka kwa Muhammad bin Ismail bin Buzeigh.
Kwa ufupi ni kwamba, wapokezi wote tuliowataja katika mlolongo huu, ni wenye kuaminika na kukubalika kisawasawa mbele ya watu wa fani ya uchunguzi wa maisha ya wapokezi wa Hadithi ijulikanayo kwa jina la (Elmur-Rijaal).
Uchunguzi juu ya wapokezi wa mlolongo huu:
Ibnu Abi Jiid: yeye huyu ni miongoni mwa walimu wa Sheikh Tusiy na marehemu Najashi, naye (Ibnu Abi Jiid) pia alikuwa ni mmoja mwenye kumhadithia marehemu Najashi Riwaya mbali mbali, yeye basi atakuwa hana dosari, kwani wanazuoni wote kwa jumla ni wenye kukubaliana na wale wote wenye kumnukulia Hadithi marehemu Najashi, kwa hiyo hakuna haja ya kupoteza wakati kwa ajili ya kuuchunguza uaminifu wa mpokezi huyu.[15]
Muhammad bin Hassan bin Waliid:
Yeye ni mmoja kati ya wanazuoni wakubwa wa madhehebu ya Kishia waliowiva vizuri katika fani ya uchunguzi wa maisha ya wapokezi wa Hadithi, kwa hiyo hakuna haja ya kumfanyia uchunguzi mpokezi huyu. Marehemu Najashi alimsifu mwanazuoni huyu kwa kusema: Abu Muhammad bin Hassan bin Ahmad bin Waliid, ni mmoja kati ya wanazuoni waku wa mji wa Qum. Yeye hana dosari ya aina yoyote ile katika uaminifu na ukweli alionao, naye ni fakhari kwetu.[16]
Ali bin Ibrahim Qummiy:
Yeye ni muaminifu katika upokezi wa Hadithi na ni mwenye kuaminiwa, pia yeye hakuwa na matatizo ya kiimani katika dini na madhehebu yake.[17]
Ibrahim bin Hashim:
Yeye alikuwa ni wa mwanzo aliyezieneza Hadithi za watu wa mji wa Kufa ndani mji wa Qum, naye ni miongoni mwa waandishi walioandika vitabu tofauti.[18] Mwanazuoni maarufu ajulikanaye kwa jina la Hilliy, amesema kuwa: ni vyema zaidi kuzikubali kauli za mpokezi huyu.[19]
Mlolongo na mfumo wa pili
La pili linalotaka kutafitiwa ni: mlolongo na njia ya mapokezi iliyotoka kwa Muhammad bin Ismail bin Buzeigh hadi kuishia kwa Alqama bin Muhammad Al-Hadhramiy
Muhammad bin Ismail bin Buzeigh:
Yeye ameipokea Riwaya hii kutoka kwa watu wawili, huku wao wakiwa wameipokea Riwaya hiyo kutoka kwa Alqama.
Marehemu Najashi kuhusiana na Muhammad bi Ismail bin Buzeigh amesema: mpokezi huyu anatokana na kizazi cha Hamza bin Buzeigh, naye ni miongoni mwa wafuasi wema wa Maimamu (a.s), pia yeye ni mwenye kuamainika na ni mchapa kazi mzuri.[20]
Yeye aliinukuu Riwaya hii kwa kusema: (baba yangu ameniambia kuwa: Muhammad bin Ali bin Husein amesema kuwa: Muhammad bin Ali Maajiluwie ameniambia kuwa yeye amepokea kutoka kwa… akimwambia kuwa: sisi tulikwenda kwa Imamu Ridha (a.s), katika mazungumzo yetu tukamgusia Muhammad bin Ismail Buzeigh, hapo Imamu (a.s) akasema: mimi ninapenda sana kumuona mmoja wenu akiwa na sifa kama zake yeye (Muhammad bin Buzeigh).[21] Pia Sheikh Tusiy amemtathimini mpokezi huyu kwa kusema: Muhammad bin Ismail bin Buzeigh ni muaminifu na ni mtu asiye na utata juu yake, yeye ni mtu wa mji wa Kufa aliyekuwa ni mtumishi wa Mansuur.[22]
Ama kuhusiana na wale watu wawili nao ni Saleh bin Uqba na Seif bin Umeira, ambao Muhammad bin Ismail amenukuu Hadithi kutoka kwao, inabidi kuwafafanua kwa ufafanuzi ufuatao:
Saleh bin Uqba:
Saleh bin Uqba bin Qeis ni miongoni mwa wafuasi wa Imamu Saadiq (a.s).[23] Najashi kuhusiana na mpokezi huyu anasema: Saleh bin Uqba bin Qeis bin Sam-a'an bin Abi Rubaiha, ambaye ni mtumishi wa Mtume (s.a.w.w)… .[24] Na wengine kama vile marehemu Sayyid Bahrul-uluu wamesema: kwa kutokana na kuwa Sheikh Najashi amemtaja mpokezi huyu wa Hadthi ndani ya kitabu chake, na hakumtia aina yoyote ya dosari kuhusiana na dini pamoja na madhehebu yake, hilo linaonesha kuwa yeye alikuwa ni mfuasi wa madhehebu ya Kishia.[25]
Iwapo mtu atakubaliana na mfumo kama huu wa kuwapasisha watu mbali mbali, hivyo basi yeye hatokuwa na shaka juu ya Saleh bin Uqba, kwani Saleh naye amesifiwa kiujumla na marehemu Najashi pamoja na Sheikh Tusiy, na hilo linatosha kumfanya yeye awe na sifa njema. Ingawaje hapa hakuna dalili tosha zitakazomfanya yeye akubalike moja kwa moja, lakini sisi tunaweza kumpasisha yeye kupitia njia nyengine, na njia zenyewe ni kama zifuatazo:
La kwanza kabisa ni kuwa: kuna watu muhimu na maarufu kama vile Muhammad bin Husein bin Abil-Khattaab aliyefariki mnamo mwaka 262, pamoja na Muhammad bin Buzeigh ambao wamepokea Hadithi kutoka kwa mpokezi huyu, na hilo ni moja linaloonesha uaminifu wake, kwani mtu makini kama Muhammad bin Ismail bin Buzeigh si rahisi kuweza kunukuu Hadithi kutoka kwa mtu asiyeaminika, kwani yeye alikuwa ni miongoni mwa wafuasi waliosifika mbele ya Imamu wa nane wa Kishia (a.s). Lakini Ibnu Ghadhaairiy aliyefariki mwaka 411 Hijiria amemshusha hadhi Saleh bin Uqba akidai kuwa: Saleh bin Uqba ni miongoni mwa Maghulati (wenye kuamini uungu wa Ali (a.s)), na ni mzushi asiyetegemeka.[26] Pia Allaama maeinukuu kauli hiyo katika kitabu chake.[27]
Lakini usemi na madai ya Ibnu Ghadhaairiy hayana thamani ya kielimu, kwani yeye hakuwa na mezani madhubuti ya kuwachunguza watu, bali wakati mwengine alikuwa akisikia kuwa fulani ni miongoni mwa Maghlati, naye alikuwa akiwahesabu kuwa ni miongoni mwao, hali ya kwamba katika zama alizokuwa akiishi Ibnu Ghadhaairiy, watu walikuwa wakituhumiwa kiholela tu. Marehemu Ayatul-Lahi Khui ameyakanusha madai ya Ibnu Ghadhaairiy kwa kusema: kwa kweli tuhuma zilizonukuliwa kutoka kwa Ibnu Ghadhaairiy, haziwezi kupingana na vithibitisho mbali mbali vya kumtakasa mpokezi huyu vilizonukuliwa katika vitabu, pia sisi tumetoa dalili zilizothibitisha kuwa, kitabu kinachodaiwa kuwa ni cha Ibnu Ghadhaairiy, ambacho kimempaka matope mpokezi huyu, bado hakijathibitika kitabu hicho kuwa ni cha Ibnu Ghadhaairiy.[28]
LA PILI: Sheikh Tusiy pamoja na Najashi ndani ya nukuu zao za Riwaya, kwa namna moja au nyengine wameonesha aina maalumu ya tegemeo lao kuhusiana na kitabu cha mpokezi huyu, na hilo linaonesha kuwa wao wamekipa aina maalumu ya thamani kitabu hicho, na hilo linaashiria heshima maalumu waliomuekea mpokezi huyu. Hapa twaweza kusema kuwa: mpokezi huyu ni miongoni mwa watu waliopata kiwango maalumu cha sifa zinazozifanya kauli zake kukubalika na kupata uzito. Kwa hiyo Saleh bin Uqba ni mpokezi anayekubalika, na Riwaya zake ni zenye uzito na zenye kuaminika.
Seif bin Umeira:
Seif bin Umeira Nakhaiy ni mtu muaminifu anayeaminika, naye ni mmoja kati ya wafuasi waliopokea Hadithi moja kwa moja kutoka kwa Imamu Sadiq na Imam Kadhim (a.s), Sheikh Tusiy na Najashi wameeleza wazi wazi kuwa mpokezi huyu ni muaminifu.[29]
Hivyo basi hata kama Saleh bin Uqba atakuwa si mtu aliyetakaswa na kuaminiwa na waandishi, bado hilo halitoweza kuidhoofisha Riwaya hii, kwani Muhammad bin Ismail bin Buzeigh ameipokea Riwaya hii kutoka kwa wawili hawa bila mapokezi ya wawili hawa kutegemeana katika nukuu zao, kwa hiyo kama mmoja wao atakuwa ni dhaifu asiyeaminika, hilo haliwezi kumungusha yule mpokezi wa pili mwenye kuaminika wala kuidhoofisha kauli yake katika kuinukuu Riwaya hii.
Alqama bin Muhammad Al-Hadhramiy:
Alqama ni miongoni mwa wafuasi wa Imamu Saadiq na Baaqir (a.s),[30] waandishi hawakumsifu mtu huyu kwa aina fulani ya sifa, bali Sheikh Tusiy peke yake amemzungumza mpokezi huyu kwa kusema: Alqama bin Muhammad Al-Hadhramiy Al-Kufiy ni mpokezi aliyeegemezewa kwake nukuu mbali mbali za wapokezi wa Hadithi.[31] Pia marehemu Sayyid Ali Borjudiy, ameonekana kumkosha mpokezi huyu kupitia kipengele kilichotajwa na Sheikh Tusiy pamoja na kutumia Riwaya moja nyengine kwa ajili ya kumtukuza.[32]
Pia kuna dalili nyengine zinazoweza kuuthibitisha uaminifu wa mpokezi huyu, kwani sisi baadaye pale tutapofikia hatua ya kulihakiki tegemeo na egemeo la Riwaya ya Sheikh Tusiy, tutaona kuwa pale wapokezi wawili waaminifu (Seif bin Umeira na Safwan bin Mehran) walipotatizana kuhusiana na mtindo na mpangilio wa kumtakia Sala na salamu Imamu Husein (a.s), Seif bin Umeira alimwambia Safwan: katika Riwaya ya Alqama mtindo wa Sala na salamu hizi, haukuwa kama vile usemavyo wewe, naye akamjibu kwa kumwambia: mimi nimemsikia Imamu Baaqir (a.s) akiielezea Riwaya hii katika mtindo huu ninaokwambia mimi. Mjadala huu unaonesha kuwa watu wawili hawa hawakuwa na shaka juu ya uaminifu wa Alqama, ndio maana Seif bin Umeira akaitegemea Riwaya na mapokezi ya mpokezi huyu (Alqama), huku Safwan akionekana kuto mtia dosari mpokezi huyu bali yeye alijibu kwa kusema: mimi hivi ndivyo nilivyomsikia Imamu Saadiq (a.s) kuhusiana na Riwaya hii.[33]
Kwa ibara nyengine ni kwamba, Riwaya ya Safwan inaashiria moja kwa moja usahihi wa Riwaya iliyopokelewa na Alqama kuhusiana na Sala na salamu maalumu zisomwazo katika siku ya Ashura, isipokuwa yeye anatofautiana na Alqama katika mpangilio wa Sala na salamu hizo zilivyo, mpangilo ambao yeye Safwan amesema kuwa ameupokea kutoka kwa Imamu Saadiq (a.s). Pia Kashi katika kitabu chake amenukuu majadiliano kuhusiana na Riwaya hii yaliyotokea baina ya Safwan na nduguye (Abu Bakar Al-Hadhramiy) pamoja na Zeid bin Ali, na nukuu hii imeashiria kuwa ndugu hawa wawili walikuwa ni watu waaminifu wenye kukubalika ambao walikuwa wakiishi ndani ya zama za Imamu Saadiq (a.s).[34]
Hadi hapa tayari tumeshafahamu kuwa Riwaya hii ni yenye kukubalika na kutegemeka. Lakini Sheikh Tusiy ameinukuu Ziara ya Ashura katika mtindo mwengine usiokua huo, nao ni kama ufuatao:
2- Mapokezi ya Riwaya hii kupitia kwa Sheikh Tusiy
Muhammad bin Khalid Tayaalisiy amemnukuu Seif bin Umeira akisema: mimi pamoja na Safwan bin Mehran Jammaal tukiwa pamoja na baadhi ya wafuasi wengine tulielekea Najaf. Na baada ya kumaliza Ziara yetu (Sala na salamu kwa Imamu Ali (a.s)), Safwan aliuelekeza uso wake ule upande aliozikwa Imamu Husein (a.s) ndani yake (yaani Karbala), kisha akatuambia: elekeeni upande huu wa kichwani mwa kaburi la Imamu Ali (a.s), kwa ajili ya kumsalia na kumtakia amani Imamu Husein (a.s), kwani pale mimi nilipokuwa pamoja na Imamu Saadiq (a.s), nilimuona Yeye (a.s) akiwa amesimama na kuelekea upande huu, kisha akamsalia na kumtakia amani Imamu Husein (a.s), hali mimi nikiwa pamoja Naye (a.s). Seif anaendelea kunukuu kwa kusema: kisha Safwan akaisoma Ziara ile ile (Sala na salamu) ambayo Alqma bin Muhammad Al-Hadhramiy ameinikuu kutoka kwa Imamu Baaqir (a.s) kuhusiana na siku ya Ashura, hapo Seif bin Safwan akamwambia: baadhi ya vipengele vya Riwaya ulioisoma havimo ndani ya ile Riwara iliyonukuliwa na Alqama kutoka kwa Imamu Baaqir (a.s)! yeye akamjibu: mimi Ziara hii nimeisikia kutoka kwa Imamu Saadiq (a.s).[35]
Dhahiri ya Riwaya hii ni kuwa Imamu Saadiq (a.s) alielekea upande wa Karbala na kuisoma Ziara ile ile ambayo Alqama ameinukuu kutoka kwa Imamu Baaqir (a.s).
Kuhusiana na egemeo na tegemeo linaloonekana katika katika mapokezi ya Riwaya hii kupitia mtindo huo hapo juu, kwa kweli sisi hatuoni aina yeyote ili ya utata ndani yake, kwani Seif bin Umeira na Safwan ni wapokezi walioaminika,[36] ila tu kinachotakiwa kuhakikiwa ndani ya egemeo na tegemeo hili ni mambo mawili, la kwanza ni mtiririko wa mapokezi unaoanzia kwa Sheikh Tusiy hadi kumfikia Muhammad bin Khalid Tayaalisiy, na la pili ni kumhakiki Muhammad bin Khalid Tayalisiy na kuutafuta uaminifu wake kutoka kwa wataalamu wa fani ya Hadithi.
mtiririko wa mapokezi unaoanzia kwa Sheikh Tusiy hadi kumfikia Muhammad bin Khalid Tayaalisiy
Kuna aina mbili za mitazamo kuhusiana na mtiririko huu ambayo inaweza kuzingatiwa katika njia ya kuwatakasa wapokezi walitajwa ndani mtiririko wa wapokezi wa Riwaya hii:
Mtazamo wa kwanza: ni ule unaomuangalia Muhammad bin Khalid kuwa yeye ndiye msimulizi wa Riwaya hii, pia kwa upande mwengine ibara za mtindo wa mapokezi haya zinaonesha kuwa msimulizi sio yeye bali ni mtu mwengine ndiye anayesimulia kutoka kwa Muhammad bin Khalid.
Kule kuiegemeza Riwaya hii kwa kwa Muhammad bin Khalid Tayaalisiy, ni jambo lisilokuwa na mashaka, kwani hilo limethibitishwa na Kheikh Tusiy, kwa hiyo mtiririko wa mapokezi haya utakuwa ni wenye kuthibiti na kuaminika.
Mtazamo wa pili: ni ule wenye kuona kuwa: Sheikh Tusiy ameinukuu Riawaya hii kutoka katika kitabu cha Muhammad bin Khalid Tayaalisiy, na maandiko yanaonesha kuwa Riwaya hiyo, imenukuliwa na Husein bin Ubeidil-Lahi Ghadhairiy, naye ameinukuu kutoka kwa Ahmad bin Muhammad bin Yahya Attaar, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Muhammad bin Ali bin Mahbuub, kutoka kwa Muhammad bin Khalid Tayaalisiy, hivyo basi Muhammad bin Ali bin Mahbuub ndiye aliyeinukuu Riwaya hii moja kwa moja kutoka kwa Muhammad bin Khalid Tayaalisiy.[37] Wapokezi waliotajwa ndani ya mtiririko huu, wote ni watu wenye kuaminika, yaani egemeo na tegemeo la Sheikh Tusiy lililoegemezwa kwenye kitabu cha Muhammad bin Khalid Tayaalisiy, ni tegemeo lenye kiwango kikubwa cha uamininikaji. Hata hivyo sisi hatutosheki na uaminikaji tu wa tegemeo na egemeo hilo, bali durubini yetu itawachunguza moja kwa moja wapokezi wote waliomo ndani ya mtirirko uliotajwa na Sheikh Tusiy. Uhakiki juu ya wapokezi hawa ni kama ifuatavyo:
Husein bin UbeidiL-lahi Ghadhairiy
Mpokezi huyu ni miongoni mwa walimu wa Sheikh Tusiy na marehemu Najashi.[38] Hapo mwanzo tulisema kuwa: walimu (wale ambao Najashi amenukuu Hadithi kutoka kwao) wote ni watu wenye muaminika, na hilo ni jambo lilithibitisha na kukubalika mbele ya wanazuoni wote wa Kishia, kwa hiyo wao hawahitajii tena kupata takaso la uaminifu kwa mara nyengine mpya. Marehemu Khui amempa dhamana ya uaminifu mpokezi huyu kwa kusema: "yeye ni miongoni mwa mashekhe wa Najashi, na sote tunatambua kuwa: walimu wa Najashi wote ni wenye kuaminika na kutegemewa na wanazuoni mbali mbali."[39]
Ahmad bin Muhammad bin Yahya Attaar
Ili kuuthibitisha ukweli na uaminifu wa mpokezi huyu, inatubidi tuegemee katika dalili zifuatazo:
A- Yeye ni miongoni mwa walimu wa marehemu Sheikh Saduq (r.a), naye (Sheikh Saduq) amepokea Riwaya mbali mbali kutoka kwa mpokezi huyo, na kinachoonekana katika ibara za Sheikh Saduq ni kwamba: kila pale alipolitaja jina la mpokezi huyu alikuwa akimuombea dua kwa kusema:
((رضی الله عنه na hilo ni lenye kuonesha ridha ya Sheikh Saduq juu ya ukweli na uaminifu wake, maneno hayo basi ndiyo yanayotuondolea shaka juu ya uaminifu wa mpokezi huyu.
B- Yeye ni miongoni mwa mashekhe wa ijaza (مشایخ الاجازه),[40] na wengi miongoni mwa wanazuoni ni wenye kuwathamini na kuwaamini wale mashekhe wote wa ijaza, kwa hiyo mashekhe wa ijaza ni wenye kukubalika na kuaminika. Mhakiki Bahraniy kuhusiana na hilo ameandika maneno yafuatayo: "mashekhe wa ijaza ni wenye daraja ya juu kabisa ya uaminifu na ni wenye hadhi na daraja kubwa."[41] Yeye ameendelea kwa kusema: "kuwashakia mashekhe wa ijaza ni jambo lisilokubalika hata kidogo."[42]
C- Wananazuoni wengi ni wenye kuziunga mkono Riwaya zilizopokelewa na mpokezi huyu, wao wamemtakasa kwa utakaso wa ukweli na uaminifu, na miongoni mwa wanazuoni waliomtakasa, ni Majlisiy, yeye katika bayana zake ameandika maneno yafuatayo: "Ahmad bin Muhammad bin Yahya Attaar, ni miongoni mwa mashekhe wa ijaza, na wanazuoni wamezisifu Riwaya zake kwa sifa ya ukweli, pia Sheikh Tusiy amenukuu Riwaya kutoka kwa mpokezi huyu kupitia kwa Ibnu Ghadhairiy na Ibnu Abi Jeid.[43]
Allaama Hilliy naye katika kitabu chake Khulaasatul-aqwaal, ameitakasa na kuikubali ile milolongo yote miliwi ya wapokezi wa Riwaya hii iliotegemewa na Sheikh Saduq katika kuinukuu Riwaya hiyo, mlolongo mmoja ukiwa umeinukuu kutoka kwa Abdur-Rahmaan bin Abi Najraan, na wa pili ukiwa umeinukuu kutoka kwa Abdul-Lahi bin Abi Ya'afuur, huku Ahmad bin Muhammad bin Yahya Attaar akiwa ni kiungo katika milolongo miwili hiyo. Hilo basi ni lenye kuonesha dhana njema ya Allaama Hilliy juu ya uaminifu wa mpokezi huyo.[44]
Kwa kweli ufafanuzi huu hauwezi kubakisha hata chembe ya shaka juu ya ukweli na uaminifu wa mtu huyu.
Muhammad bin Yahya Al-Attaar
Yeye alikuwa ni sheikhe wa Koleniy, na Sheikh Koleiniy amepokea Riwaya nyingi kutoka kwa mpokezi huyu. Marehemu Najashi akimzungumzia mpokezi huyo alisema: "Muhammmad bin Yahya ambaye umaarufu wake ni Abu Jaa'far Al-Attaar Al-Qummiy, alikuwa ni sheikh muaminifu katika zama zake ambaye wafuasi wenzetu walikuwa wakinukuu kutoka kwake, naye alikuwa ni mweingi wa Riwaya."[45] Sheikh Tusiy naye amesema: "Muhammad bin Yahya Al-Attaar ni mpokezi ambaye Sheikh Koleiniy alikuwa akinukuu kutoka kwake, naye alikuwa ni mwingi wa Riwaya."[46]
Muhammd bin Ali bi Mahbuub
Mpokezi huyu alisifiwa na Marehemu Najashi kwa kauli ifuatayo: "Muhammad bin Ali bin Mahabuub Al-Ash-a'riy Al-Qummiy, mwenye umaarufu wa Abu Jaa'far, alikuwa ndiye sheikh wa masheikh wa mji wa Qum ndani ya enzi zake, yeye alikuwa ni muaminifu mwenye kutegemewa, pia alikuwa ni mwanafiqhi aliyeshikamana kisawasawa na Madhehebu yake.[47]
Muhammad bin Khalid Tayaalisiy
Ili tuweze kuuthibitisha uaminifu wa Muhammad bin Khalid Taayalisiy, inatubidi kwanza kuviashiria vipengele vifuatavyo:
A- Muhammad bin Ali Mahbuub ambaye ni miongoni mwa wanazuoni wenye hadhi kubwa katika madhehebu ya Kishia, amenukuu Hadithi kutoka Muhammad bin Khalid Tayaalisiy, hilo basi linaashiria hali ya ridhaa yake juu ya mpokezi huyu (Muhammad bin Khalid Tayalisiy).
B- Muhammad bin Khalid Tayaalisiy, ameonekana kuwa ni kiungo muhimu ndani ya milolongo mbali mbali ya wapokezi wenye kuamainika waliotajwa ndani ya vitabu misingi vya fani ya Hadithi vyenye kuaminika.
Miongoni mwa wale wenye vitabu msingi, ni Seif bin Umeira na Muhammd bin Maa'ruuf, wao basi ndani ya vitabu vyao wamemnukuu Muhammad bin Razzaaz ambaye ni mwanachuoni mwenye kutegemeka, akinukuu Riwaya kutoka kwa Muhammad bin Khalid Tayaalisiy, na hilo ni moja kati ya dalili zinazoonesha uaminifu na utegemekaji wa Muhammad bin Khalid Tayaalisiy mbele ya mtazamo wa Razzaaz. Pia mwanachuoni mwengine ni Ruzeiq bin Zubeir, ambaye Abdul-Lahi bin Jaa'far Humeiriy amenukuu Riwaya kutoka kwake ambayo yeye (Ruzeiq bin Zubeir), ameinukuu Riwaya hiyo kutoka kwa Muhammad bin Khalid Tayaalisiy. Pia Hamiid bin Ziyaad aliyetakaswa na Sheikh Tusiy na Najashi, amepokea Riwaya chungu nzima kutoka kwa Muhammad bin Khalid Tayaalisiy.
C- Si hao tu tuliowataja hapo juu ndiyo walionukuu Riwaya kutoka kwake, bali bado kuna wengi miongoni mwa wapokezi wenye kuaminika ambao wamenukuu Riwaya kutoka kwa mpokezi huyu, na baadhi yao ni: Sa'ad bin Abdil-Lahi, Ali bin Suleiman Al-Zuraariy, Muhammad bin Hasan Saffaar, Muhammad bin Husein pamoja na Mua'wiya bin Hakiim.[48]
D- Sheikh Tusiy kuhusiana na Muhammad bin Khalid Tayaalisiy amesema: "Muhammad bin Khalid Tayaalisiy, alikuwa akiitwa kwa jina Aba Abdi-Lahii, na kuna maandiko mengi ya Hadithi yaliyopokewa kutoka kwake."[49] Ni wazi kuwa usemi huu wa Sheikh Tusiy, ni wenye kumpa yeye hadhi ya kumtukuza na kumpa sifa njema zenye kuuthibitisha wema wake.
Ithibati mbali mbali tulizozitaja kuhusiana na Muhammad bin Khalid Tayaalisiy, ni tosha katika kuutihibitisha ukweli wake, hata Ibnu Ghadhairiy ambaye alionekana kuto kuwa makini katika kuwatilia mashaka baadhi ya wapokezi, hakuonekana kumtosa Muhammad bin Khalid Tayalisiy katika jopo la madhaifu wasioaminika. Kwa hiyo hakuna kilichobakia katika uhakiki juu ya Muhammad bin Khalid Tayaalisiy. Kwa msingi huu, watu watafahamu kuwa mapokezi ya Riwaya kuhusu Zaiara ya Ashura yaliyonukuliwa kupitia Muhammad bin Khalid Tayaalisiy, ni sahihi yasio na dosari.
Mpaka hapa tayari tumeshafanya uhakiki wa kutosha kuhusiana na milolongo miwili au mategemeo na maegemeo mawili yaliyotegemewa na Sheikh Tusiy katika kuinukuu Riwaya inayozungumzia Sala na salamu maalumu zisomwazo katika siku ya Ashura, na tumefikia natija ya kuwa: mlolongo wa tegemeo na egemeo la kwanza ni sahihi lisilo na mashaka, na wala hakuna njia imara ya kutomkubali Alqama bin Muhammad bin Hadhramiy. Ama kuhusiana na mlolongo wa tegemeo na egemeo la pili, ni kwamba wapokezi wote waliomo katika jopo la mlolongo huo ni wenye kukubalika na wenye kuaminika, isipokuwa Muhammad bin Khalid Tayaalisiy, lakini pia Riwaya za Muhammad bin Khalid Tayaalisiy ni zenye kukubalika kwa kiasi fulani, kwani wanazuoni wakuu mbali mbali wa fani ya Hadithi, walikuwa wakinukuu Riwaya zao kutoka kwake.[50]
Hitimisho
Haidhuru katika Riwaya hizi tulizozinukuu, kuwa kuna baadhi ya wapokezi ambao ni wenye kutiliwa mashaka kidogo, ingawaje mashaka yao bado hayajathibitika kisawasawa, lakini bado kunaweza kukatokea watu watakaoona kuwa wapokezi hao si wenye kukubalika. Lakini tukiangalia katika milolongo yote ya wapokezi wa Riwaya hizi, tutakuta ndani ya kila mlolongo kuwa kuna wale wapokezi wasafi wenye kuaminika ndani yake, na hilo ni jambo tosha linalotufanya kuzikubali na kuziunga mkono Riwaya hizi.
[1] Kaamiluz-ziaaraat, cha Jaa'far bin Muhammad Quulewaihi, uk/325 hadi 328, chapa ya mjalada mmoja ya Mardhawiyya, Najaful-ashraf, mwaka 1356 Hijiria.
[2] Kaamiluz-ziaraat, uk/37
[3] Wasaailush-Shia cha Hurrul-Aa'miliy, juz/3, uk202, faida ya tano katika hitimisho la kitabu hicho.
[4] Miongoni mwa wanazuoni wa Karne mbili zilizopita, kuna wanazuoni wanaoona kuwa mlolongo mzima wa wapokezi wa Riwaya hiyo ni wenye kuaminika, lakini pia kuna wanazuoni wengine kama vile Ayatu-Llahi Jaa'far Subhani wanoona kuwa anayeaminika hasa miongoni mwa wapokezi waliomo ndani ya mlolongo huo ni yule tu mpokezi wa mwanzo aliyetajwa ndani ya mlolongo huo.
[5] Siratun-najaat, cha Khui, ju/2, uk/457.
[6] Tahdhibu cha Sheikh Tusiy, juz/6, uk/41. Muujamu Rijaalul-Hadith, juz/2, uk/186.
[7] Neno mashekhe hapa lina maana ya watu ambao wanategemewa na Ibnu Quulewahi katika kunukuu kwake Hadithi kutoka kwao.
[8] Khaatimatu Mustadrakul-Wasaaili, juz/3, uk/251 hadi 256, chapa ya kwanza ya Muasasatu Aalul-Baiti Qum, mwaka 1416 Hijiria.
[9] Rejea kitabu Muujamu Rijalil-Hadithi, juz/15, uk/207. Rijaalun- Najashiy, uk/348. Feherestet-Tusiyy, uk/174 na uk/410.
[10] Muujamu Rijalil-Hadithi, juz/17, uk/283.
[11] Muujamu Rijalil-Hadithi, juz/11, uk/156.
[12] Muujamu Rijalil-Hadithi, juz/14, uk/156 hadi 158.
[13] Misbahul-Mijtahidi cha Sheikh Tusiy, kilichoko katika mjalada mmoja, uk/772, chapa ya kitengo cha Fiq-hush-Shia, Beirut, mwaka 1411 Hijiria.
[14] Fehrest cha Sheikh Tusiy, uk/140, namba/594.
[15] Muujamu Rijalil-Hadithi, juz/15, uk/250.
[16] Rijalun-Najashi, uk/383, na nukuu ya maneno hayo kwa lugha ya Kiarabu ni kama ifuatavyo:
محمد بن الحسن بن أحمد بن الولید أبو جعفر شیخ القمیین ، وفقیههم ، ومتقدمهم ، ووجههم . ویقال : إنه نزیل قم، وما کان أصله منها . ثقة ثقة، عین، مسکون إلیه.
[17] Rijalun-Najashi, uk/260. Rijalu Ibnu Daawud, uk/237. Alkhulasa cha Hilliy, uk/100.
[18] Rijalun-Najashi, uk/16. Feherest cha Tusiy, uk/12.
[19] Al-Khulasa cha Hilliy, uk/5.
[20] Sifa za mpokezi huyu zimetajwa kwa lugha ya Kiarabu kama ifuatavyo:
محمد بن إسماعیل بن بزیع أبو جعفر مولى المنصور أبی جعفر، وولد بزیع بیت، منهم حمزة بن بزیع . کان من صالحی هذه الطائفة وثقاتهم، کثیر العمل؛ محمد بن اسماعیل ... .
[21] Nukuu za mazungumzo hayo imekuja katika lugha ya Kiarabu kama ifuatavyo:
[21]. أخبرنا والدی رحمه الله قال: أخبرنا محمد بن علی بن الحسین قال : حدثنا محمد بن علی ما جیلویه ، عن علی بن إبراهیم، عن أبیه ، عن علی بن معبد ، عن الحسین بن خالد الصیرفی . قال : کنا عند الرضا علیه السلام، ونحن جماعة ، فذکر محمد بن إسماعیل بن بزیع ، فقال : " وددت أن فیکم مثله "؛
Rejea kitabu: Rijalun-Najashi, uk/330 hadi 332.
[22] Rijalut-Tusiy, cha Sheikh Tusiy, uk/364.
[23] Rijalu Sheikh Tusiyy, mlango unaohusiana na wafuasi wa Imamu Saadiq (a.s), uk/138.
[24] Rijalun-Najashi, uk/200.
[25] Fawaaidur-rijaaliy cha Sayyid Bahrul-uluum, juz/4, uk/111 hadi 116.
[26] Ibnu Ghadhaairiy, juz/1, uk/69.
[27] Al-khulaasa, uk/230.
[28] Muujamu Rijalul-Hadithi, cha Sayyid Khui, juz/10, uk/85 hadi 86. Maneno hayo yamenukuliwa kwa lugha ya Kiarabu kama ifuatavyo:
أقول: لا یعارض التضعیف المنسوب إلى ابن الغضائری ، توثیق علی بن إبراهیم ، لما عرفت غیر مرة من أن نسبة الکتاب إلى ابن الغضائری لم تثبت ، فالرجل من الثقات . معجم رجال الحدیث ، السید الخوئی ، ج 10 ، ص 85 – 86.
[29] Al-Feherest cha Sheikh Tusiy, uk/140. Rijalun-Najashiy, cha Najashi, uk/189.
[30] Rijalu Tusiy, uk/140 na 262.
[31] Rijalu Tusiy, cha Sheikh Tusiy, uk/ 262.
[32] Taraaiful-maqaal, cha Sayyid Ali Borjurdiy, juz/1, uk/527.
[33] Misbahul-mutahajjid, uk/777 hadi 781.
[34] Rijalu Kashi, uk/416 hadi 417.
[35] Misbahul-mutahajjid, uk/777.
[36] Rijalun-Najashi, uk/198.
[37] Al-feherest cha Sheikh Tusiy, uk/421, namba/649.
[38] Rijalut-Tusiy, cha Sheikh Tusiy, uk425. Jijalun-Najashi, cha Najashi, uk/69.
[39] Muujamu rijalul-Hadithi, cha Sayyid Khui, juz/7, uk/23.
[40] Mashekhe wa ijaza ni wale wanazuoni wa zamani ambao walikuwa ndiyo ngazi ya kuwafikishia watu wa zama za baadae, Riwaya mbali mbali kutoka kwa Maimamu (a.s), kwa hiyo kazi yao ilikuwa ni kuwanukulia watu Riwaya na kuwapa ijaza (ruhusa) ya wao pia kuwanukulia wengine hadi ziwafikie wale watu wa kizazi cha baadae.
[41] Mi'iraju ahlul-kamaal, uk/44. Nukuu hii imekuja kwa lugha ya Kiarabu kwa mtindo ufuadtao:
مشایخ الإجازة فی أعلى طبقات الوثاقة والجلالة . معراج أهل الکمال، ص 44.
[42] Mi'iraju ahlul-kamaal, uk/88. Fawaaidur-rijaaliyya, uk44. Nukuu hii imenukuliwa kutoka katika lugha ya Kiarabu kama ifuatavyo:
إنّه لا ینبغی أن یرتاب فی عدالة شیوخ الإجازة. معراج أهل الکمال، ص 88 . برای آگاهی بیشتر نک: الفوائد الرجالیّة، ص 44، المطبوع فی آخر
رجال الخاقانی؛ الشهید الثانی، ص 192 – 193؛ میرداماد محمد باقر الحسینی الأستر آبادی، ص 261.
[43] Al-wajiza fi-elmir-rijaali, uk/154.
[44] Arria'aya fi-elmid-diraya, uk371
[45] Rijalun-Najashi, cha Najashi, uk/353.
[46] Rijalut-Tusiy, cha Sheikh Tusiy, uk439.
[47] Rijalun-Najashi, cha An-najashi, uk/349.
[48] Muu'jamu rijalul-Hadithi, juz/17, uk/76.
[49] Rijalut-Tusiy cha Sheikh Tusiy, uk/441.
[50] Aazarkhishiy diigar az aasimane Karbala, cha Muhammad Taqiy Misbahu Zazdiy.