advanced Search
KAGUA
19848
Tarehe ya kuingizwa: 2012/05/12
Summary Maswali
nini maana ya itikafu
SWALI
nini maana ya itikafu
MUKHTASARI WA JAWABU

Neno (itikafu) kilugha, huwa lina maana ya kule mtu kukaa na kubaki katika sehemu au pahala maalumu, huku akiwa ameshikamana na jambo maalumu ndani ya mahala hapo, lakini neno hili kitaalamu (kwenye fani ya sheria za Kiislam) linamaanisha kule mtu kukaa katika sehemu takatifu kwa ajili ya kutaka kujikaribisha kwa Mola wake. Itikafu si jambo maalumu lililovumbuliwa na Uislamu, na wala si jambo ambalo lipo kwenye dini ya Kiislam tu, bali jambo hili pia lilikuwepo katika dini mbali mbali zilizopita, kisha ulipokuja Uislamu ukaliendeleza na kulipa nguvu, pia yawezekana kuwa baadhi ya sheria zake zimebadilishwa na dini hii ya Kiislam. Itikafu huwa haina muda maalumu, lakini lililo muhimu na la lazima katika itikafu ni kufunga saumu, kwa hiyo ni lazima mtu anapotaka kukaa itikafu, achaguwe zile siku ambazo zinaruhusiwa kufunga saumu ndani yake. Hivyo basi zama zozote zile ambazo saumu huwa inajuzu ndani yake, itikafu pia itakuwa ni yenye kujuzu katika siku hizo, lakini nyakati bora zaidi kwa ajili ya itikafu, ni zile siku za ndani ya kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani, au ndani ya masiku meupe ya mwezi wa Rajabu. Na kuna sehemu maalum ambazo zinaruhusiwa kufanya ibada hii ya itakafu. Kauli maaru kuhusiana na mahala pa kufanyia itikafu ni kwamba: ibada hii inatakiwa kufanywa ndani ya mmoja kati ya misikiti minne, nayo ni: msikiti wa Makka, msikiti wa Madina,  Masjid Kufa na Masjid Basra. Lakini kuna wanazuoni wengine wambao wamesema kuwa: inafaa pia kufanya itikafu katika kila msikiti mkuu wa mji au mahala fulani.

JAWABU KWA UFAFANUZI

Neno (itikafu) kilugha, huwa lina maana ya kule mtu kukaa na kubaki katika sehemu au pahala maalumu, huku akiwa ameshikamana na jambo maalumu ndani ya mahala hapo, lakini neno hili kitaalamu (kwenye fani ya sheria za Kiislam) linamaanisha kule mtu kukaa katika sehemu takatifu kwa ajili ya kutaka kujikaribisha kwa Mola wake.

Itikafu ni moja kati ya mambo muhimu ambayo yanamsaidia mtu kuto jisahau katika ulimwengu wenye hadaa na wa mpito, ulimwengu ambao kila mmoja wetu huwa ni rahisi kupotea ndani yake, kwa hiyo itikafu ni fursa nzuri ya mja kuutafuta ukaribu wa Mola wake pamoja na kumuomba Mola huyo amvue na amuepushe na giza la dunia.

 

Historia ya itikafu

Itikafu si jambo maalimu na makhususi kwa dini ya Kiislamu peke yake, bali itikafu pia ilikuwepo ndani ya dini zilizopita, kisha Uislamu ukaliendeleza jambo hilo, ingawaje yawezekana ibada hii ikawa na aina fulani ya mabadiliko abayo yamefanya na Uislamu.

Tangu Mtume (s.a.w.w) alipowafundisha Waislamu ibada ya itikafu, ibada hii imekuwa ni ibada maarufu ndani ya Uislamu.

Katika zama hizi ibada hii imekuwa ni ibada maarufu ambayo hutiliwa mkazo ndani ya nchi mbalimbali za Kiislamu, na linapoingia kumi la mwisho la Ramadhani, nchi mbali mbali kama vile Saudi Arabia, Iran pamoja na nchi nyengine, huwa zinawatayarishia wananchi wake matayarisho maalumu kwa ajili ya ibada hii, pia watu mbali mbali kutoka nchi tofauti vijana pamoja na wazee, humiminika kwenye msikiti wa Makka kwa ajili ya kufanya itikafu ndani ya msikiti huo, na wacha Mungu wengi ambao wana nia ya kufanya ibada ya umra, huamua kufanya ibada zao za umra ndani ya kumi hilo kwa ajili ya kupata fadhila hizo za itikafu. Pia ibada hii hufanyika ndani ya msikiti wa Mtume (s.a.w.w) ulioko Madina. Na waumini wengi wa madhehebu ya shia wanahudhuria katika misikiti hiyo, huku wengine huelekea Masjid Kufa na Masjid Basra kwa ajili ya kutekeleza ibada hiyo muhimu ya itikafu.

 

 

 

 

Thamani ya itikafu

Kumuabudu Mola na kujiepusha na hadaa za dunia ni jambo muhimu lililotiliwa mkazo ndani ya ibara mbali mbali za dini, na itikafu katika kumpelekea mja kumuabudu Mola ni yenye kukamata nafasi ya mwanzo ndani ya ibada mbali mbali ziwezazo kumuamsha mja kutokana na usingizi wa dunia, na kuna Hadithi mbali mbali zinazohimiza kufanya ibada ya itikafu na kushikamana na ibada hiyo. huku Qur-ani pia ikilitilia mkazo jambo hilo.

Mola katika Qur-ani Anasema: “Na tukamuamuru Ibarahim na Isamail (a.s) kuitayarisha nyumba yetu (Kaaba) kwa ajili ya wenye kukaa itikafu ….”[1]

Itikafu ni yenye masharti maalumu, na baadhi yake zimetajwa kwenye Aya nyengine isiyokuwa hii.[2]

 

 

Wakati wa kufanya itikafu

Itikafu haikuwekewa wakati maalumu, lakini kwa kutokana na kuwa saumu ni moja kati ya masharti ya itikafu, kwa hiyo ni lazima yule anayetaka kufanya ibada hii, aangaliye ni masiku gani ambayo mja huruhusiwa kufunga, na ndani ya masiku hayo ndiyo afanye itikafu yake, lakini pia kuna masiku malumu ambayo ni yenye kupendekezwa zaidi kufanya ibada ya itikafu ndani yake, nayo ni: ndani ya kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani na ndani ya masiku meupe ya mwezi wa Rajabu. Itikafu ndani ya kumi la mwisho la mwezi wa Ramadhani ni yenye fungamano la moja kwa moja na kumpa mja yale matayarisho yatakayomuwezesha yeye kufanya ibada kwa juhudi za hali ya juu ndani ya masiku ya Lailatul- Qadri.

Kuhusiana na ibada ya itikafu hadithi zinatuelezea kuwa: Mtume (s.a.w.w) alikuwa akifanya ibada ya itikafu katika kumi lote la mwisho la mwezi wa Ramadhani,[3] na katika mwaka ambao Mtume (s.a.w.w) hakuhudhuria kwenye itikafu kwa sababu ya vita, katika mwaka uliofuata aliamua kukaa itikafu kwenye makumu yote mawili ya mwisho wa Ramadhani, kwa nia ya kulilipa lile kumi la mwaka uliopita ambalo hakuweza kukaa itikafu ndani yake kwa sababu ya vita.[4] Na ndani ya nchi ya Irani watu wamezoea kukaa itikafu katika siku tatu za mwisho za mwezi wa Rajabu na siku kumi za mwisho za mwezi wa Ramadhamani.

 

Siku tatu za mwisho za mwezi wa Rajabu ni zenye umuhimu kwa sababu zifuatazo:

1- mwezi wa Rajabu ni miongoni mwa miezi mitukufu, na linaloeleweka kutoka katika Hadithi ni kwamba: itikafu ndani ya miezi mitukufu huwa na thamani zaidi kuliko ndani ya miezi iliyobakia.

2- kufunga ndani ya mwezi wa Rajabu ni jambo lenye fadhila mno, hii ni kwa kutokana na utukufu wa mwezi huu, na hata katika zama za kijahili watu walikuwa wakiutukuza mno mwezi huu. Na Uislamu nao umezidi kuuzingatia utukufu wa mwezi wa Rajabu.[5] Kinachoonekana ni kwamba: suala la kuutukuza mwezi wa Rajabu, ni moja kati ya masuala ambayo yalikuwa yakizingatiwa na dini mbali mbali zilizopita.

 

Sehemu ya kufanyia ibada ya itikafu

Itikafu inatakiwa kufanywa katika maeneo maalumu. Kauli maarufu kuhusiana na sehemu ya kufanyia ibada hii, ni ile isemayo kuwa: ibada hii inatakiwa kufanywa kwenye mmoja kati ya misikiti mikuu minne, nayo ni: Masjidil-Haraam (msikiti wa Makka), Masjidin-Nabiy (s.a.w.w), Masjidi Kufa na Masjidi Basra. Imam Ridha (a.s) amesema:

“Fadhila za kukaa itikafu ndani ya msikiti wa Mtume karibu na kaburi Lake (.s.a.w.w), ni sawa na fadhila zinazopatikana katika ibada ya hija na umra.”[6] Lakini pia baadhi ya wanazuoni wamejuzisha kukaa itikafu ndani ya kila msikiti mkuu wa mji fulani au mahala fulani.[7]

Lakini kuhusiana na itikafu ifanywayo kwenye misikiti mikuu ya mji au mahala fulani, kuna wanazuoni waliosema kuwa: itikafu hiyo iantakiwa kufanywa huku mtu akiwa na matarajio ya kuwa huenenda Mola akaikubali ibada hiyo, na siyo kuweka yakini juu ya ibada hiyo kuwa ni yenye kukubalika kisawasawa.[8]

Kufanya itikafu kwenye misikiti mbali mbali iliyoko kwenye viambo au kwenye sehemu mashuhuri, si jambo lenye kukubalika na wanazuoni wengi wa Kishia, bali kuna kidogo tu miongoni mwa wanazouni wa Kishia wenye kukubaliana na kauli hiyo.[9] Inaposemwa kuwa: mtu anaweza kufanya itikafu kwenye misikiti mikuu ya mji au mahala fulani, huwa inakusudiwa ile misikiti ambayo watu wengi hukusanyika ndani yake kwa ajili ya kufanya ibada zao.[10] Na kwa kauli nyengine ni kwamba hapo hukusudiwa ile misikiti ambayo mara nyingi huwa ndiyo yenye kujaa watu zaidi kuliko misikiti mengine.[11]

Hapa mtu anaweza kuuliza kuwa: kwa kutokana na umuhimu wa ibada hii, je si vizuri wanazuoni wakawaruhusu watu kufanya ibada ya itikafu katika misikiti yote? Kwani kufanya hivyo ndiko kutakowafanya watu wengi kuweza kuitekeleza kirahisi ibada hiyo, jawabu ya swali hili ni kama ifuatavyo: masula ya ibada ndani ya dini ya Kiislamu, ni mambo ambayo hayawezi kutiwa mkono na mtu fulani, bali ibada hizi huwa zinatakiwa kubakia kama vile zilivyopokelewa kutoka kwenye maandiko na ibara zilivyo.

Pia tunatakiwa kufahamu kuwa: kuna baadhi ya ibada fulani ambazo msingi wake mkuu huwa ni kule kuzifanya ibada hizo katika mahala maalumu panapohusika, na mfano wa ibada hizo ni ili ibada ya hija. Kwa hiyo haiwezekani ibada ya hija kukubalika bila ya kuifanya ndani ya eneo lake husika, ambalo ni moja kati ya misingi mikuu ya ibada hiyo.

Suala la itikafu nalo endapo litathibiti kuwa ni lenye kujuzu kutekelezwa kwenye misikiti mikuu, hapo tutatakiwa kufahamu kuwa: Mola ametutaka kuifanya ibada hiyo katika eneo hilo na sio eneo ambalo sisi wenyewe tutalichagua, na ingawaje sisi tutakuwa hatufahamu umuhimu na maslahi yaliyoifanya ibada hiyo kutakiwa kufanya kwenye maeneo hayo maalumu, lakini bila shaka Mola huwa hafanyi jambo bila ya kuyaangalia maslahi ya jamii ya Kiislamu na ulumwengu kwa jumla.

Labda pengine Mola alitaka kuwaweka Waislamu katika sehemu moja na kuwakusanya pamoja, huku akiwavuta ili kuwanya wawe kitu kimoja.[12][13]

 


[1] Suratul-Baqara Aya ya 125.

[2] Suratul-Baqara Aya ya 187.

[3] Imeilezewa na Mhammad Husein Hurrul- Aamiliy, katika kitabu Wasailu Shia, juz/10, uk/5336, hadithi ya 14046, ambacho kimechapishwa na Muasasatu Aalu Bait, Qum Iran, chapa ya mwaka 1409 Hijiria.

[4] Kitabu kilichopita, hadithi ya 14047.

[5] Fadhailu- Ash-huri talatha, cha sheikh Saduqu, uk/24, Hadithi ya 12.

[6] Biharul-Anwaar, juz/98, uk/151.

[7] Urwatul-Wuthqaa cha Sayyid Muhammad Tabaatabai, mlango wa itikafu, uk/399.

[8] Tahrirul-Wasila cha imam Khomeiniy, juz/1, uk/305.

[9] Jawahirul-Kalaam, cha sheikh Muhammad Hassan Najafiy, juz/17, uk/170.

[10] Kitabu kilichopita, uk/171.

[11] Majmaul-Masaail, cha Ayatullahi Gulpeiganiy, juz/1, uk/154.

[12] Biharul-Anwaar, juz/33, uk/542.

[13] Mtayaridhaji ni Ismail Nasaji Zawaare, kwa kuchukua fira kutoka tovuti ya Hawza Net.

 

TARJAMA YA JAWABU KATIKA LUGHA NYENGINE
MAONI
Idadi ya maoni 0
Tafadhali ingiza thamani
mfano : Yourname@YourDomane.ext
Tafadhali ingiza thamani
<< Niburute.
Tafadhali ingiza kiasi sahihi ya usalama Kanuni

MPANGILIO WA KIMAUDHUI

MASWALI KIHOLELA

YALIYOSOMWA ZAIDI