advanced Search
KAGUA
9706
Tarehe ya kuingizwa: 2012/05/23
Summary Maswali
ibara ya laana yenye kuulenga ukoo wa Banu Umayya, haitoacha kumgusa mwana wa Yazidu, kwani naye ni miongoni mwa watu wa ukoo huo, vipi basi sisi tukubaliane na Ziara hiyo na kukadai kuwa ni maandilo sahihi yatokayo kwa Maimamu (a.s)?
SWALI
ibara ya laana yenye kuulenga ukoo wa Banu Umayya, haitoacha kumgusa mwana wa Yazidu, kwani naye ni miongoni mwa watu wa ukoo huo, vipi basi sisi tuweze kukubaliana na Ziara hiyo huku tukidai kuwa ni maandiko sahihi?
MUKHTASARI WA JAWABU

Ndani ya ibara zilizomo kwenye maandiko ya Sala na salamu za siku ya Ashura zijulikanazo kwa jina la Ziaratu-Aa'shuuraa, kuna ibara ya kuwalaani Banu Umayya wote kwa ujumla akiwemo mwana wa Yazidu. Huku baadhi ya wanatarehe mbali mbali wakionekana kuwatakasa baadhi ya watu wa ukoo wa Banu Umayya akiwemo mwana huyo wa Yazidu, wana tarehe hao wamefanya hivyo kwa kuona baadhi ya huduma mbali mbali zilizotolewa na watu hao, jambo ambalo linaonekana kupingana na zile ibara za laana zilizowaelekea watu wa ukoo huo.

   Ili kuutibu mgongano unaopatikana katika kauli za kusifka kwao na zile ibara za laana zenye kuonekana kuuelekea ukoo mzima wa wtu wa Banu Umayya, inabidi kila mmoja wetu afahamu ya kuwa:

  Ibara za laana ni zenye kuwakusudia wale tu waliowaunga mkono madahlimu wa Banu Umayya kifikra, kimatendo, na kiimani, watu ambao ima walishiriki moja kwa moja katika dhulma za kupingana na Uimamu (Ukhalifa) wa kizazi cha Mtume (s.a.w.w), au walikuwa ni wenye kufunga mikono na kushuhudia dhulma hizo bila kujali, au pia wale waliokuwa wakishangiria na kufurahi kwa matokeo ya dhulma hizo, dhulma ambazo ziliishia katika kuwaua Maimamu pamoja na wafuasi wao (a.s). Ukweli huu unaweza kubainika baatu ya mtu kuvitafakari vizuri vipengele vya Ziara hiyo vilivyo , kwani laana zote zilizokuja ndani ya Ziara hiyo zimeelekezwa kwa wale waliokikalia kiti cha Uimamu, kiti ambacho kilikuwa ni nafasi maalumu kwa watu wa nyumba ya Mtume tu (s.a.w.w). Madhalimu hawa walikuwa na nia ya kuizima taa ya Mola Mtukufu kwa midomo yao, ambo walitumia kila zana kwa ajili ya kuuboresha uwadui wao dhidi ya watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w), pia laana hizo zimewagusa moja kwa moja wale wote waliowaunga mkono katika hilo, ambao walikuwa na ridhaa juu ya kupatikana kwa aina kama hiyo ya ugaidi. Hivyo basi watu wema waliomo ndani ya ukoo wa Banu Umayya,  wao otomatiki watakuwa wako nje  ya laana hizo zilizoelekezwa kwenye ukoo huo, hii ni kwa sababu tokea mwanzo maandiko na matamshi hayo yalipowaelekea watu madhalimu wa Banu Umayya, yaliwakengeuka wale wote walio wema miongoni mwa watu wa ukoo huo, na sio kwamba matamshi hayo mwanzo yalitamkwa kiujumla jamala na kukusudiwa watu wa ukoo mzima, kisha ndipo kukatafutwa mbinu ya kuwakiuka au kuwakengeuka wale wema miongoni mwao.

JAWABU KWA UFAFANUZI

Jawabu ya swali lako inabidi kuitafuta ndani ya uhakiki wa vitu viwili tofauti: cha kwanza ni kumhakiki mwana wa Yazidu katika nyanja mbali mbali za kiimani na kiamali (kimatendo), na cha pili ni kuihakiki maana ya ibara za laana zilizotajwa ndani ya Ziara ya Ashura pamoja na kuyatafiti makusudio yake ya kuwalani watu wa ukoo wa Banu Umayya kiujumla.

Uhakiki juu ya mwana wa Yazidu

Kuhusiana na uhakiki juu ya mwana wa Yazidu, yapasa kusema kuwa: hatua iliyochukuliwa na mwana wa Yazidu ajulikanaye kwa jina la Muawia, katika kutaka kumtenga na kumueka mbali baba yake na kiti cha ukhalifa, ilikuwa ni hatua njema inayostahiki kushukuriwa, kwani yeye alifahamu mapema ule unyang'anyi wa nafasi hiyo ambayo ilikuwa ni nafasi ya watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w), lakini hilo halitoshi kutufanya sisi kumuhesabu yeye kuwa ni miongoni mwa watu wema, hasa tukizingatia kuwa sisi hatuna yakini juu ya uhakika na nia kamili ya tendo lake hilo, pia hatuna uhakika wa kuwa yeye alitubia mbele ya Mola wake kutokana na matendo yake mabaya aliyoyatanguliza, na wala hatuna yakini kuwa je yeye ni mhusika aliyehusishwa ndani ya ibara hizo za laana au yeye yuko nje ya ibara hizo? Kosa la kukalia kiti cha ukhalifa bila ya haki ni miongoni mwa makosa makubwa mno, hata kama tendo hilo litakuwa ni tendo la kipindi cha mpito tu, na bila shaka usamehevu juu ya tendo hilo utakuwa ni wenye kuzingatia masharti maalumu ya toba. Shaka ya yeye kuwa ni mtu mwema aliyekubalika mbele ya Mola wake itazidi kuwa ni jambo lenye utata, hasa pale sisi tunapoiangalia kauli ya Imamu Sajjaad (a.s) kuhusiana na Omar bin Abdul-Aziiz, kwani imepokewa Riwaya kutoka kwa Imamu Sajjaad (a.s) ya kuwa Imamu Sajjaad (a.s) alimwambia Abdul-Lahi bin Ataa "…Huyu (Omar bin Abdul-Aziiz) atakufa huku akililiwa na watu wa ardhini, hali akiwa ni mwenye kulaaniwa na wale walioko mbinguni."[1] Hii inatokana na yeye kukikalia kiti cha ukhalifa cha watu wa nyumba ya Mtume (s.a.w.w) pasi na haki, ingawaje yeye alionekana kuwa ni mbora zaidi ya wale waliopita kabla yake, ingawaje pia sisi hatuna ushahidi wa kusema kuwa Muawia bin Yazidu au Omar bin Abdul-Aziiz ni miongoni mwa watu wilio kataliwa moja kwa moja na Mola wao.[2] Kwa vyovyote vile sisi hatuwezi kujua vipi Mungu atawahukumu, bali Mola tu ndiye Mjuzi wa hatima yao, lakini kuna baadhi ya watu wanaotokana na ukoo wa Banu Umayya huku wakiwa ni watu wema, na hilo si jambo linalopingika, kwani miongoni mwao kulikuwa kuna watu waliokuwa ni wafuasi wa Ahlu-Bait (a.s), na baadhi yao ni Muhammad bin Said bin Aa's na Abul-A'as bin Rabii' pamoja na Said bin Kheir.

  Kwa kutokana na kuwa kuna miongoni mwa watu wa ukoo wa Banu Umayya waliojulikana kwa wema na hisani, hivyo ni lazima kuihakiki ibara inayowalani Banu Umayya ndani ya Ziara ya Ashura.

Uhakiki juu ya laana kwa Banu Umayya kiujumla

Kabla ya sisi kuanza tafiti kuhusiana na suala hili, ni muhimu kwanza watu wafahamu kuwa; Mola hamuadhibu mja wake kwa kutokana na dhambi za wengine, na wala Yeye hawalaumu waja wake au kuwatikisa kwa mitikiso ya kidunia au ya Akhera kwa kutokana na dhambi wasizozitenda, isipokuwa pale wao wanapokuwa ni wenye aina fulani ya mchango iliyochangia kutokea dhambi hizo, au kuwa na moyo mkunjufu juu ya matokeo ya dhambi hizo au kuzinyamazia kimya dhambi hizo zitokeapo.

 Kwa hiyo hatoadhibiwa mja na Mola wake ila yule atakayeshiriki katika matokeo ya dhambi kwa namna moja au nyingine kama tulivyofafanua hapo juu, kwa hiyo adhabu yaweza kumuendea mja kwa aina kama hiyo ya makosa, na sio kwa kutokana na makosa ya wengine.[3]

  Ngamia wa Nabii Saleh (a.s) aliuliwa na mmoja tu miongoni mwa watu wa Thamudu, hali ya kuwa pale Qur-ani inapokizungumzia kisa hicho, haimtaji tu yule muuaji wa ngamia huyo, bali huwahesabu watu wote wa Thamudu kwa ujumla kuwa ni wenye makosa katika tokeo hilo na ni wenye kustahiki adhabu kutokana na tendo hilo, hii ni kwa sababu  ya wao kulinyamazia kimya tendo hilo, kimya ambacho kiliashiria ridhaa na furaha juu ya mauaji ya ngamia wa Nabii Saleh (ngamia wa Mungu),[4] kama vile alivyosema Ali (a.s) kuhusiana na kisa hicho: "wao (watu wa Thamudu) walishiriki katika tendo hilo kupitia chuki za ndani ya nyoyo zao juu ya ngamia huyo, na pia baada ya mauaji ya ngamia huyo, walijawa na furaha ndani kwa ndani, chuki na furaha hizo za pamoja ndizo zilizowapelekea wao kupata adhabu ya aina moja."[5] Kwa mtazamo wa Qur-ani, mezani na kigezo kikuu cha kuwahesabu watu au mtu Fulani kuwa ni mfuasi au ni miongoni mwa watu wa kabila fulani, ni kule kuwepo uwiano wa kifikra na nyenendo baina yake na kabila au gurupu alilolinganishwa nalo, na hatiame kuhesabiwa kuwa ni miongoni mwao.

   Kwa mwenye kutaka kufahamu vizuri kuhusiana na hilo, basi na ayaangalie maneno ya Mola kuhusiana na mwana wa Nabii Nuhu (a.s), Mola alimwambia Nuhu (a.s): "Kwa hakika yeye (huyo mwanao) si miongoni mwa watu wako..".[6] Kule mwana wa Nabii Nuhu kuwekwa nje ya wafuasi wa Nabii Nuhu, kunatokana na ile hali ya kutokuwepo fungamano la amali zenye kwenda sawa na fikra za Nabii huyo, angalia basi jinsi ya Mola alivyo mtenga mtoto huyu, hali yeye akiwa ni mwenye uhusiano wa damu na Nabii Nuhu (a.s), na kwa upande wa pili, muangalie Mtume wa Mola (s.a.w.w) jinsi alivyomueka Suleiman Farisiy ubavuni mwake na kumuhesabu kuwa ni miongoni mwa watu wa nyumba yake (s.a.w.w).[7]

Kwa hiyo Maimamu hawawaehesabu wale watu wema waliomo ndani ya ukoo wa Banu Umayya kuwa ni miongoni mwa Banu Umayya, na dhihiriko hasa la ukweli huu linaakisika kutoka katika kisa cha Saa'dil-Kheir aliyelia kama mtoto mdogo mbele ya Imamu Muhammad Baaqir (a.s), Yeye (a.s) alivyomuona katika hali ile akamuuliza: ni nini kinachokuliza? Saa'd akamjibu: kwa nini nisilie hali ya kuwa mimi ni miongoni mwa ule mti (ukoo) uliolaaniwa!? Hapo basi Imamu (a.s) akamwambia: wewe si miongoni mwao, bali wewe unatokana na ukuu wao tu huku ukiwa ni miongoni mwetu, kwani wewe hujasikia kauli ya Mola Mtukufu isemayo: "Yule atakayenifuata mimi huyo ni miongoni mwa watu wangu".[8]

   Ufafanuzi huu tulioutoa hapa unakusudia kusema kuwa, wanaokusudiwa katika ile laana inayowaelekea watu wa Bunu Umayya, ni wale tu wenye matendo na fikra ziendazo sawa na fikra za madhalimu wa Banu Umayya, watu ambao ima walihusika moja kwa moja, au walikuwa ni wenye kushuhudia hali wakizinyamazia kimya dhulma hizo, au pia kuzifurahia kwa namna fulani. Na maana hii ni yenye kuonekana wazi wazi ndani ya vipengele vya ibara za Ziara ya Ashura, kwani laana hizo nimeelekezwa moja kwa moja kweye lile kundi la Banu Umayya au lile kundi ambalo lilijaribu kutumia nguvu katika kukikalia kiti cha Ukhalifa kinyume na haki, huku wao wakiwa na nia ya kuizima nuru ya Mola Mtukufu kwa kutokana na chuki zao juu ya kizazi cha Mtume (s.a..w.w). Pia laana hizo zinawahusu moja kwa moja wale walioziunga mkono dhulma hizo kwa namna moja au nyengine. Kwa hiyo kuvuka na kukaa nje ya laana hizo wale watu wema wa Banu Umayya, kunatokana na kule laana hizo kuto waelekeaa wao tokea mwanzo, kwani tokea mwanzo ibara za laana hizo zilikuwa haziwaelekei wala haziwahusu watu wema, watu hao wawe wamo ndani ya ukoo wa Banu Umayya au nje ya ukoo huo.

Marehemu Abul-Fadhli Mirza Tehraniy amelifafanua vyema suala hilo katika uchambuzi na ufafanuzi wake wa Ziara ya Ashura, yeye alipkuwa akisisitiza ukweli na uhakika wa laana hizo, alitumia ibara mbili zifuatazo kuwa ni kama dalili za yale ayasemayo:

1- Laana zilizokuja katika Ziara ya Ashura zimejikita na kujifunga kwenye kundi maalumu lenyekutambulika vyema kwa dhulma zake, yaani laana hizo ziliwahusu wale madhalimu huku zikiwavua wasiokua madhalimu ndani ya ukoo wa Banu Umayya.

2- Maimamu walionekana kuitumia ibara ya (Banu Umayya) huku wakiwalenga Abu Sufyan, Muawia na Aalu-Maruwaan katika usemi wao huo.[9]

Natija kamili ya uhakiki

Sasa tayari tumeshatambua uhakika wa laana na namna ya laana hizo zinavyowahusisha baadhi na kuwaepuwa kutoka katika jiko la laana hizo wale wasiohusika miongoni mwa watu wa ukoo wa Banu Umayya, hivyo basi iwapo itathibiti kuwa Muawia mwana wa Yazidu ni miongoni wa watu wema, basi laana hizo hazitomuelekea wa kumhusisha yeye na kumtumbukiza ndani ya jungu hilo kuu la laana juu ya ukoo wa Banu Umayya.

 

[1] Basaairud-darajaat, cha Muhammad bin Hassan  Saffaar, uk/170, chapa ya pili ya Qum mwaka 1404 Hijiria.

[2] Kutokana na kutokuwa na uhakika juu ya usafi wa Omar bin Abdul-Aziiz, kuna baadhi ya wanazuoni kama vile Mirza Abdul-Lahi Afandiy, wenye utata juu ya kujuzu au kuto juzu laana kwa ajili ya Omar bin Abdul-Aziiz, pia Sayyid Radhiy ndani ya kitabu chake cha mombolezo, kuna kipande cha mashairi yaliyomsifu na kumheshimu Omar bin Abdil-Aziiz.

[3] Suratun-Najmu, Aya ya 38 hadi 41. Israa Aya ya 18. Faatir Aya ya 7.

[4] Suratu Qamar, Aya ya 29. Tafsiri ya Nahjul-balagha ya Subhiy Saleh, khutba ya 201, uk/319. Suratu Aa'raaf, Aya ya 77. Huud, Aya ya 65. Ahua'raa, Aya ya 157. Shamsu, Aya ya 14.

[5] Nahjul-balagha, khutba ya 201, uk/319.

[6] Suratu Huud, Aya ya 46:

"قالَ یا نُوحُ إِنَّهُ لَیْسَ مِنْ أَهْلِکَ إِنَّهُ عَمَلٌ غَیْرُ صالِحٍ فَلا تَسْئَلْنِ ما لَیْسَ لَکَ بِهِ عِلْمٌ إِنِّی أَعِظُکَ أَنْ تَکُونَ مِنَ الْجاهِلینَ"

[7] Bihaarul-anwaar, cha Muhammad Baaqir Majlisiy, juz/65, uk/55, chapa ya Alwafaa, Beirut, mwaka 1404 Hijiria.

[8] Bihaarul-anwaar, cha Muhammad Baaqir Majlisiy, juz/46, uk/337.

[9] Mirza Abul-Lfadhli Tehraniy kwenye kitabu chake Shifaus-suduur fi sherhe Ziaraat Ashura, juz/1, uk/255 hadi 263, chapa ya kwanza ya Murtadhawiy, mwaka 1376 Shamsia.

 

TARJAMA YA JAWABU KATIKA LUGHA NYENGINE
MAONI
Idadi ya maoni 0
Tafadhali ingiza thamani
mfano : Yourname@YourDomane.ext
Tafadhali ingiza thamani
<< Niburute.
Tafadhali ingiza kiasi sahihi ya usalama Kanuni

MPANGILIO WA KIMAUDHUI

MASWALI KIHOLELA

YALIYOSOMWA ZAIDI