Please Wait
10902
Kuna baadhi ya vitabu vya Tarehe vilivyoeleza kuwa: ingawaje Yazidu alikuwa ana kila aina ya starehe alizozitayarisha kwenye nyumba yake, wakiwemo aina mbali mbali za wanawake, lakini bado alikuwa hatosheki, na hakuwa akiyafumba macho yake pale anapowaona wanawake waliojistiri wakitembea mitaani au wakiwa katika kazi zao za kila siku, hivyo jicho lake likawa limeangukia kwenye mwanamke mcha-Mungu aliye na haya zake, mwanamke ambaye alijulikana kwa jina la Urainab bint Is-haaq, ambaye alikuwa ni mke wa Abdu-Llahi bin Salaam.
Muawiya ambaye ni baba wa Yazidu alifanya aina mbali mbali za ujanja ili amuchishe mwanamke huyo kutoka kwa mumewe, kisha amuunganishe na mwanawe (Yazidu) aliyejulikana kwa wingi wa uchafu na maasi. Imamu Husein (a.s) aliugundua ujanja na hila za Muawiya, hivyo basi akafanya kila juhudi ili ampiku Muawiya katika ujanja wake huo, na hatimae akaweza kuipangua mipango hiyo ya Muawiya, na baada ya muda si mrefu, kwa kupitia njia sahihi za sheria ya Kiislamu, akamrejesha mwanamke huyo kwa mumewe, hapo basi mwanamke huyo mwema na kizazi chake wakaweza kuepukana na ukoo mchafu wa Yazidu.
Ingawaje kuna aina mbali mbali za upungufu zinazoonekana katika vitabu vyenye kunukuu kisa hichi, lakini hata kama tutakihisabu kisa hicho kuwa ni cha kweli, kisa hicho hakitoweza kumtia aina fulani ya dosari Imamu Husein (a.s), bali kitakuwa ni miongoni mwa sifa njema zenye kuonesha ushupavu wa kisiasa pamoja na huruma alizonazo Imamu Husein (a.s), katika kuistiri jamii ya Kiislamu.
Hakuna hata kitabu kimoja cha Tarehe kilicho madhubuti, chenye kunukuu kisa hicho na kukihesabu kuwa ni moja kati ya sababu za chuki zilizosababisha kupatikana kwa vita vya Karbala.
Kinachoonekana ndani ya baadhi ya vitabu vya Tarehe ni kwamba: ndani ya zama za utawala wa Muawiya, kulikuwepo mwanmke mwema aliyejulikana kwa jina la (Urainab) bint Is-haaq, mwanmke ambaye alisifika sana kwa uzuri wa tabia na maumbile.
Yazidu mwana wa Muawiya ambaye katika zama hizo alikuwa ni naibu wa baba yake katika ukhalifa, alimpenda sana mwanamke huyo, ama kabla ya yeye kufanya matayarisho ya kwenda kumposa, tayari (Urainab) akawa ameshafunga ndoa na mwana wa ami yake (Abdu-Llahi bin Salaam) ambaye alikuwa ni mtu maarufu katika zama hizo, Urainab na mumewe walikuwa wakiishi katika ardhi ya Iraq kwa raha na furaha.
Muawiya alitambua kuwa mwanawe alikua akimpenda Urainab, hapo akampa kauli mwanawe ya kufanya kila njia ili ayatimize matilaba ya mwanawe. Katika zama hizo Abdu-Llahi alikuwa na jukumu maalumu la kazi alilopewa na Muawiya huko Iraq. Muawiya alimtaka Abdu-Llahi aende Sham (Syria) mji amboa ulikuwa ndiyo maakazi ya utawala wa Muawiya. Muawiya alimtuma Abu-Dardaa na Abu-Huraira waende kumwambia kuwa: Muawiya anakuita ili aukuozeshe bint yake; kwani wewe ndiye unayestahili kuwa ni mkwe wa khalifa.
Abdu-Llahi alikubaliana na ushauri huo, kisha Abu-Huraira na Abu-Dardaa wakafanya haraka kumjuilisha Muawiya hali inavyokwenda. Hapo Muawiya akamwambia bint yake kuwa: “iwapo Abu-Huraira na Abu-Dardaa wataleta posa ya Abdu-Llahi, basi wewe kubali! Lakini waambie kuwa mimi niko tayari lakini kwa sharti ya Abdu-Llahi kumuacha mkewe” hapo basi Abdu-Llahi akahadalika na akakubali kumuacha mkewe, kisha akamtaka Muawiya kuto kwenda kinyume na kauli yake.
Muawiya alimjibu: “iwapo bint yangu ataridhia, mimi sina tatizo”. Baada ya yeye kumuacha mkewe, Abu-Dardaa na Abu-Huraira wakaenda kwa bint ya Muawiya kumpa habari za kuwa Abdu-Llahi tayari ameshamuacha mkewe, hapo bint wa Muawiya akajibu: “kwa kweli kwanza inabidi nifikiri, kisha nitafute ushauri kuhusiana na suala hili la ndoa”.
Muda ukapita na Urainab akawa tayari ameshamaliza eda ya talaka yake. Abu-Dardaa na Abu-Huraira wakaenda tena kumsikiliza bint wa Muawiya, lakini bado hawakupata jawabu muwafaka, na badala yake akawajibu kuwa: “ndoa hii kwa kweli haina maslahi nami”!! na hapo ndipo Muawiya alipomtuma Abu-Dardaa aende Iraq kwa ajili ya kumposea Yazidu Urainab. Baada ya Abu-Dardaa kufika Iraq, alifahamu kuwa Imamu Husein (a.s) yupo hapo Iraq katika mji wa (Kuufa), hapo basi aliamua kwanza kwenda kwa Imamu Husein (a.s) kisha aelekee kwenye ujumbe aliotumwa kuutekeleza. Abu-Dardaa alipofika kwa Imamu Husein (a.s), Imamu akamuuliza: umekuja kufanya nini? Abu-Dardaa akamuelezea Imamu kile alichokijia, hapo Imamu (a.s) akamwambia: “kwa kweli hata mimi nilkuwa na niya ya kumtuma mtu aende kwa Urainab kwa ajili ya posa. Kwa hiyo kama unakwenda kwa Urainab, basi salamu zangu pia zifikishe kwake.” Abu-Dardaa alipofika kwa Urainab akazifikisha posa zote mbili kwa pamoja, hapo Urainab akamtaka ushauri Abu-Dardaa kwa kumwambia: “ni posa ipi iliyo bora zaidi miongoni mwa hizi mbili?” Abu-Dardaa akamjibu: “ni bora zaidi Imamu Husein (a.s) kuwa ndiye mumeo”.
Imamu (a.s) akatoa kauli ya kiwango kile kile ambacho Yazidu alikuwa akitaka kutoa na kumpa Urainab kwa ajili ya mahari, kisha akafunga ndoa na Urainab.
Muawiya akaanza kukata fungamano na Abdu-Llahi bin Salaam na hatimae akaacha kumlipa mshahara, hapo basi Abdu-Llahi ambaye alikuwa akiishi huko Syria kikazi, akaamua kurudi kwa mkewe (Urainab) ili akachukuwe kiwango fulani cha amana ambacho alikuwa amekiweka kwake, moja kwa moja akaenda kwa Imamu Husein (a.s) na kumuelezea kuwa amekuja kwa ajili ya kuchukua amana yake aliyokuwa ameiweka kwa mkewe wa mwanzo. Alipofika kwa Urainab, yeye alishindwa kuuzuia moyo wake akawa amejawa na huzuni, na Urainab naye akawa yuko katika hali kama hiyo, hapo wote wawili wakawa wanalizana, Imamu Husein (a.s) alivyoiona hali ile, alijawa na huruma kisha akasema: “sawa basi mimi nimeshamuacha Urainab talaka tatu. Ewe Mola shuhudia kuwa mimi sikumuoa kwa kutokana na uzuri au mali aliyokuwa nayo, bali nilimuoa kwa kajili ya kumhifadhi hadi atakapokuja mumewe”. Kisha Imamu akatoa amri ili Urainab apewe mahari aliyokuwa amemuahidi kumpa. Urainab na mumewe wakataka kukataa kuchukuwa mahari hayo, ili iwe ni kama shukurani maalumu ya kukishukuru kitendo chema cha Imamu (a.s), lakini Imamu (a.s) akawaambia: “thawabu nitakazozipata ni bora kuliko mali”, hapo Urainab na mumewe wakaendelea kuishi kama kawaida.[1]
Kuna mambo mabali mbali yenye kuonyesha udhaifu wa tokeo hilo. Na baadhi ya mambo hayo ni kama iffuatavyo:
1- Hadithi yenye kuzungumzia suala hilo ni Haddithi mursal, na wala Hadithi hiyo haina aina yoyote ile egemezo kuhusiana na mapokezi yake, kwani Ibnu Qutaiba (muandishi wa kitabu maarufu Al-Imama wa Siasa) ni miongoni mwa waandishi wa Qarne ya tatu Hijiria, naye alizaliwa mwaka 213 Hijiria huko (Kuufa), na Imamu Husein (a.s) aliuwawa mwaka 61 Hijiria huko Karbala. Hivyo basi Ibnu Qutaiba alizaliwa baada ya miaka 152 baada ya kuuwawa Imamu Husein (a.s), na kisa hicho anachokinukuu, ni kisa kinachonukuliwa kutokea kabla ya yeye kuzaliwa, kwa hiyo inambidi yeye kukinukuu kisa hicho kutoka kwa watu wailoishi katika zama za kisa hicho, lakini yeye hakukinukuu kisa hicho kutoka kwa watu hao, na hata kama atakuwa yeye amekinukuu kutoka kwa watu fulani, lakini yeye hakuwataja watu hao, jambo ambalo linatufanya sisi kutoweza kukifanyia uchunguzi kisa hicho katika usahihi wake.
2- Abu-Dardaa ambaye ametajwa ndani ya kisa hicho akiwa ni kama kiungo baina ya Muawiya, Abdu-Llahi bin Salaam na Urainab, ni mtu ambaye anaaminika kuwa amefarika ndani ya zama za ukhalifa wa Otham. Na wengi miongoni mwa Wanatarehe wameandika kuwa yeye alifariki miongoni mwa mwaka 38 na 39 Hijiria.[2] Vipi basi yeye anaweza kuwa ni kiungo cha tokeo hilo ambalo linatarajiwa au kubuniwa kuwa limetokea katika zama za mwishoni mwa ukhalifa wa Muawiya?
3- Tokeo hili halionekani kunukuliwa na vitabu muhimu vya Tarehe. Bali kitabu muhimu kilicholinukuu tokeo hili ni kitabu (Al-Imaama wa Siasa), kitabu ambacho bado kuna watu wanaokitilia mashaka kuhusina na kuwa je ni Ibnu Qutaiba ndiye aliyekiandika kitabu hicho au la?[3]
4- Hakuna hata andiko moja lenye kuaminika linaloonesha kuwa Imamu Husein (a.s) alikwenda Iraq baada ya Kuuwawa baba yake (Ali (a.s)), kisha kuelekea Madina, isipokuwa katika zama za tokeo la Ashura, lakini maelezo yaliyodai kutokea kisa hicho cha Urainab yanaonesha kinyume na hivyo.
5- Ndani ya kisa hichi imenukuliwa kuwa Imamu Husein (a.s), alimuacha Urainab talaka 3 kwa pamoja, hali ya kwamba haiwezekani mtu kumuacha mkewe talaka tatu kwa pamoja, na wala suala hilo halikubaliki kisheria, na iwapo mtu atamuacha mkewe talaka tatu kwa pamoja, basi itahesabiwa kuwa ni talaka moja tu katika sheria ya Kiislamu.[4]
6- Moja kati ya sharti za kusihi kwa talaka, ni kuwepo kwa mashahidi wawili. Mola Mtukufu katika Qur-ani Anasema: “Na washuhudie mashahidi wawili miongoni mwenu, na msimamishe ushahidi huo kwa ajili ya kumtii Mola wenu.”[5] Na Imamu Saadiq (a.s) anasema: “Hakuna talaka inayosihi ila kwa kuwepo mashahidi wawili”.[6] Lakini katika kisa kilichonukuliwa hapo juu, hakuonekani kuwepo kwa shahidi pale imamu alipomuacha Urainab.
Kila kimoja miongoni vipengele tulivyovitaja hapo juu, kinatosha kuwa ni sababu ya kutotiliwa maanani kisa hiccho, lakini pia iwapo tutavifumbia macho vipengele vyote hivyo tulivyovitaja, na kukihesabu kisa hicho kuwa ni kisa cha kweli, basi hakuna dosari yoyote ile itakayomuelekea Imamu Huein (a.s), bali kisa hicho kitakuwa ni muongozo wa sababu za watu kuutambua uungwana, imani na siasa njema alizokuwa nazo Imamu Husein (a.s), pamoja na huruma alizukuwa nazo katika kuitetea na kuihifadhi jamii ya Kiislamu.
Riwaya hii inaonyesha vile Imamu Husein (a.s) alivyomuokoa yule mwanamke mwema kutaka katika mikono ya kishetani na hatimae kumrejesha kwa mumewe. Na Riwaya hii imetilia mkazo kuwa Imamu Husein (a.s) alisema: “Ewe Mola, Wewe unatambua vya kutosha kuwa mimi sikumuoa Urainab kwa ajili ya mali na uzuri wake…”, na baada tu ya Imamu (a.s) kuwaona kuwa bado wao wanapendana, aliamua kumrejesha mwanamke huyo kwa mumewe kwa kule kumpa talaka.
Mazingatio makubwa ya Imamu Husein (a.s) katika kuwatetea wanyonge, yanaonekana wazi kabisa katika Riwaya hii.
Na jengine linalopaswa kuzingatiwa ni kwamba, hakuna hata nukuu moja yenye kuamanika inayonukuu kuwa tokeo hilo lilikuwa ni miongoni mwa sababu zilizochangia kutokea vita vya Karbala.
Kwa ajili ya utafiti zaidi, rejea kitabu (Al-Imaama wa Siasa).
[1] Al-Imama wa Siasa cha Ibnu Qutaiba.
[2] Rejea Al-kaamilu fi taariikh cha Ibnu Athiir, juz/3, uk/129, chapa ya Daaru Saadir, Beirut Lebanon, mwaka 1385 Hijiria sawa na mwaka 1995 Miladia, pia Istiiaab cha Abdul-Barr, juz/3, uk/1229 na 1230, chini ya utafiti wa Muhammad Al-Bajaawiy, chapa ya Daaarul-Jiil, Beirut Lebanon, chapa ya kwanza ya mwaka 1414 Hijiria sawa na mwaka 1992 Miladia, pia Al-Isaaba fii tamyiizi sahaaba cha Ibnu Hajar Asqalaaniy, juz/4, uk/622, chini ya utafiti wa Aadil Ahmad Abdul-Maujuud na Ali bin Muhammad Muawwidh, chapa ya Daarul-Kutubil-Ilmiyya, Beirut Lebanon, chapa ya kwanza ya mwaka 1415 Hijiria sawa na mwaka 1995 Miladia.
[3] Daairatul-Maarif ya Kiislamu (Daairatu-Maarif Bozorge Islaamiy), juz/10, makala namba 3918 (Al-Imaama wa Siasa), chapa ya Markaze daairatul-Maari Bozorge Islaamiy, Tehran, Iran, mwaka 1376 Shamsia.
[4] Wasaailu Shia cha Hurrul-Aamiliy, juz/22, uk/21, chapa ya Aalul-Bait.
[5] Suratu Talaaq, Aya ya 2.
[6] Wasaailu Shia, juz/22, uk/25.