Please Wait
10431
Kila mwaka wa Hijiria kwa kawaida huwa una miezi kumi na mbili, na masiku ya miezi huwa yanahesabiwa kwa kuonekana kwa mwezi, hii ni kanuni ya mwaka wa Hijiria, ama mwaka Shamsia kwa kawaida masiku yake huwa tayari yameshatambulikana, na suala la kuonekana kwa mwezi si suala la mwezi wa Ramadhani tu, bali ni kanuni ya miezi yote ya mwaka wa Hijiria, kwa hiyo Ramadhani huingia kwa kuonekana kwa mwezi na humalizika kwa kuonekana kwa mwezi, na dalili juu ya hilo ni ile Haditi maarufu isemayo: “صُمْ لِلرُّؤْيَةِ وَ أَفْطِرْ لِلرُّؤْيَةِ”, yaani: “fungeni kwa kuuona mwezi na fungueni kwa kuuona mwezi”, na hiyo niyo mizani juu ya suala la Ramadhani, na wala hakuna jambo jengine. Lakini vile vile kuna Hadithi zilizozungumzia kuwa: Ramadhani ni siku thalathini, na kuna baadhi ya wanazuoni wa zamani walitoa fatwa za aina hiyo, kwa kule kuzitegemea baadhi ya hadithi, lakini tukiangalia upande wa pili tutazikutia zile hadithi ambazo ni zenye uzito zaidi na zilizo na wapokezi wengi zaidi na pia usahihi wake ni makini zaidi, na vile vile sisi hatuoni kuwa kuna tofauti baina ya miezi jinsi inavyoingia. Kwa hiyo hadithi hizo huwa ni zenye kugongana na zenye uzito zaidi, na zenye kuingia akilini zaidi, ndiyo maana wanachuoni walio wengi hawakubaliani na mtazamo huo.
Elimu ya Fiqhi ni sawa na elimu nyengine, haiwezi kufahamika na kila mtu, ina wataalamu wake maalumu, na ili mtu aweze kuichuma, ni lazima afanye jitihada za hali ya juu na ni lazima kuutolea muhanga wakati wake kwa ajili ya kusoma masomo tofauti kama vile: Nahwu, Elu rijal, Diraya, Usuli fiqhi na mengineyo, na baada ya juhudi kubwa hapo ndipo mtu anaweza kuwa ni mtaalamu wa fani hiyo. Na kila mtu wa fani anatambua kuwa si kirahisi tu mwanachuoni anaweza kushikamana na hadithi fulani, au Aya fulani, bila ya upekuzi na ujasiri maalumu.
Na kuhusina na suala lako tunapenda kukujibu kuwa: kila mwaka wa Hijiria ni wenye miezi kumi na mbili,[1] na kanuni ya kuingia na kumalizika kwa kila mmoja kati ya miezi hiyo, ni kuonekana kwa mwezi huo pale uunapoingia na kuonekana kwa mwezi unaofuata pale mwezi huo unapomalizika[2], na wala hakuna tofauti baina ya mwezi mmoja na mwengine,[3] na katika Riwaya zetu kuna hadithi isemayo:
صُمْ لِلرُّؤْيَةِ وَ أَفْطِرْ لِلرُّؤْيَةِ؛”[4] yaani tegemeo la kuingia Ramadhani ni kuonekana kwa kwezi wa Ramadhani, na tegemeo la kumalizika kwa mwezi huo ni kuonekana kwa mwezi wa Shawwal na si kitu chengine zaidi ya hilo. Lakini kwa ajili ya kukufaidisha zaidi, kwanza tumeamua kuinukuu Hadithi inayosema kuwa: mwezi wa Ramadhani ni wenye siku thalathini, na kisha tutaanza kuifanyia uchunguzi:
"عِدَّةٌ مِنْ أَصْحَابِنَا عَنْ سَهْلِ بْنِ زِيَادٍ عَنْ مُحَمَّدِ بْنِ إِسْمَاعِيلَ عَنْ بَعْضِ أَصْحَابِهِ عَنْ أَبِي عَبْدِ اللَّهِ (ع) قَالَ إِنَّ اللَّهَ تَبَارَكَ وَ تَعَالَى خَلَقَ الدُّنْيَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اخْتَزَلَهَا عَنْ أَيَّامِ السَّنَةِ وَ السَّنَةُ ثَلَاثُمِائَةٍ وَ أَرْبَعٌ وَ خَمْسُونَ يَوْماً شَعْبَانُ لَا يَتِمُ أَبَداً رَمَضَانُ لَا يَنْقُصُ وَ اللَّهِ أَبَداً وَ لَا تَكُونُ فَرِيضَةٌ نَاقِصَةً".[5]
Ndani ya Hadithi hii imesemwa kuwa: imam Sadiq (a.s) amesema kuwa: “….mwezi wa Shaabani miaka yote hautokamilika, na Ramadhani nayo haaitopunguka siku 30. Na Hadithi hii inaonekana ndiyo Hadithi muhimu inayotegemewa na wanachuoni wa upande wa pili, na ndani ya kitabu kimoja tu kinachoonyesha kuwa Hadithi hiyo ni yenye egemeo lililoegemea katika mapokezi sahihi, na haidhuru kuwa kuna vitabu vyengine vilivyoielezea Hadithi hii, lakini vimeielezea kwa kuinukuu kutoka katika kitabu hichi hichi tulichokiashiria ndani ya rejeo zetu, lakini hadithi hii imekabiliwa na matatizo mbali mbali ya kitaalamu yanayozingatiwa na fani ya Qifiqhi, na hilo ndilo lililotufanya kuachana na Hadithi hiyo, na miongoni mwa matatizo yanayoonekana kwenye hadithi hii ni kama ifuatavyo:
1- Hadithi hii inaonekana kuwa na tatizo la (irsaa), na inaitwa Hadithi mursal, nayo ni hadithi iliyonakiliwa bila ya kutajwa yule aliyeinakili. Na wakati mwenge mwenye kitabu anainakili Hadithi hii moja kwa moja kutoka kwa imam mwenyewe, bila ya kuwataja wapokezi wake, na Hadithi inaponakiliwa moja kwa moja bila ya kutajwa wapokezi wake hutwa Hadithi marfuu, naye mwenyewe kwa mwenywe ameamua kuitumia Hadithi hiyo bila ya kuiegemeza kwa mpokezi maalumu.[6]
2- La pili ni kwamba: mmoja kati ya wapokezi wa Hadithi hii ni Muhammad bin Sinan, mtu ambaye amepewa sifa mbaya katika fani ya Hadithi, na wala hakuna mtu mwenye shaka ya kuto kubalika kwa mpokezi huyu, kwa hiyo hakuna njia itakayoifanya Hadithi hii kukubalika.[7]
3-hadithi hii ni yenye kupingana na Hadithi nyingi ambazo ni sahihi, na miongoni mwa Hadithi hizo ni zile ambazo tulizonukuu katika maandiko yetu ya hapo juu, na ni jambo la wazi kabisa kuwa: iwapo Hadithi dhaifu itapingana na Hadithi sahihi, Hadithi hiyo huporomoka thamani yake na huchukuliwa ile Hadithi iliyo makini na kutumiwa. Mwanachuoni Hilli anasema: “hii ni hadithi yenye mapokezi mamoja tu yasiyo salama, na ni yenye kupingana na Qur-ani.[8]
Kwa hiyo ingawaje kuna baadhi ya wanachuoni walioitumia na kuitegemea Hadithi, lakini kwa kutokana na matatizo mbali mbali yaliyodhihirika hapo juu, Haiwezi Hadithi kukubalika na kushika nafasi ya matumizi kwenye mlango wa funga, kwa hiyo kinachozingatiwa katika uingiaji na utokaji wa miezi, ni kuonekana kwa mwezi, na hakuna tofauti baina ya mwezi wa Ramadhani na miezi mengine iliyobakia.
[1] Suratu Tauba Aya ya 36, isemayo: "إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِنْدَ اللَّهِ اثْنا عَشَرَ شَهْراً".
[2] Suratul-Baqara Aya ya 189, isemayo: "يَسْئَلُونَكَ عَنِ الْأَهِلَّةِ قُلْ هِيَ مَواقيتُ لِلنَّاس".
[3] Biharul-Anuwaar cha Muhammad Baqir Majilisi, juz/55, uk/236, pale aliponukuu kwa kusema: “ na imepokewa kutoka kwa Abi Abdillahi Al-Sadiq (a.s) kwamba amesema: “mwezi wa Ramadhani unasibiwa na upungufu na ziada kama inavyosibiwa miezi mengine””.
[4] Tahdhibul-Ahkaam cha sheikh Tusi, juz/4, uk/159, chapa ya Darul-kutubil-Islaamiyya, Tehran mwaka 1365 Hijiria Shamsia.
[5] Usulil-Kafi, juz/4, uk/78, Babu Nadir, Hadithi ya2, isemayo: “kwa kweli Mola ameiumba dunia ndani ya siku sita, kisha siku hizo akaziozulu na kuzitenga na dunia, ndiyo maana mwa ukawa na siku 354, hivyo siku zote mwezi wa Shaabani hautoandama thalathini, na naapa kwa jina la Mola kuwa Ramadhani haiwezi kupunguka siku 30.
[6] Mukhtalafu Shia Fi Ahkaami Sharia cha Husein bin Yusuf bin Mutahar, juz/3, uk/501, chapa ya kitengo cha uchapishaji cha Muasasatu Nashri Islaamiy, chenye fungamano na Jaamiatul-Mudarrisiin, chapa ya pili, Qum, mwaka 1413 Hijiria Qamaria.
[7] AL-Raddi alaa ashabil- adad cha Muhammad bin Muhammad bin Nuuman, uk/20, mlango wa jawaabatu ahlil-Muusal, Al-muutamarul- aalamiy lialfiyyati Sheikhil- Mufid, Qum, chapa ya kwanza ya mwaka 1413 Hijiria.
[8] Mukhtalafu Shia fii ahkami Sharia, juz/3, uk/501.