advanced Search
KAGUA
15918
Tarehe ya kuingizwa: 2010/04/06
Summary Maswali
je ni kweli kuwa Maimamu ni wabora zaidi kuliko hata Mitume?
SWALI
Imamu Khomeiniy kwenye kitabu chake (Hukuumate Islaamiyye) amesema: “kwa kweli daraja za Maimamu ziko juu kweli, kiasi ya kwamba si Malaika wala Mitume wanaoweza kuzifikia daraja hizo. Usemi huo upo kwenye uk/25 wa kitabu hicho. Ni vipi basi yeye ameweza kuyasema maneno mazito kiasi hicho, na vipi maneno hayo yanaweza kukubalika?
MUKHTASARI WA JAWABU

Suala la Maimamu (a.s) kuwazidi Mitume katika daraja za kielimu, ni suala moja linalo onekana kuzungumziwa sana na Riwaya mbali mbali, na sababu hasa za wao kuwazidi Mitume kielimu, zinatokana na ule uhakika wa nuru ya maumbile yao, kwani uhakika wa nuru yao unatokana na uhakika wa nuru ya Mtume (s.a.w.w), kwa hiyo hakuna tofauti baina ya nuru ya Mtume (s.a.w.w) na nuru ya Maimamu hao (a.s). Bila shaka Mtume (s.a.w.w) ni mbora kuliko wote, hivyo basi Maimamu nao (a.s) watakuwa ni wabora kuliko wote, hii ni kwa kutokana na lile fungamano la nuru lililopo baina yao, pia suala la mwanaadamu kuwa ni mbora kuliko Malaika, ni suala lililokubalika mbele ya Waislamu wote, kwa hiyo hakuna dalili ya wao kutokuwa wabora zaidi ya Malaika.

JAWABU KWA UFAFANUZI

Imamu Khomeiniy (r.a) hakuyasema maneno hayo bila ya mashiko maalumu, bali maneno hayo ameyatoa kutoka kwenye vitabu vya Hadithi. Miongoni mwa Hadithi zinazolizungumzia suala hilo, ni hadithi iliyonukuliwa kupitia mlolongo wa wapokezi maalumu kwa mtindo ufuatao: kutoka kwa Ahmad bin Muhammad, kutoka kwa Muhammad bin Husein, kutoka kwa Mansuur bin Abbaas, kutoka kwa Safwaan bin Yahya, kutoka kwa Abdu-Llahi bin Maskaan, kutoka kwa Muhammad bin Abdul-Khaaliq na Abi Basiir, wao wamesema: “Abu Abdi-Llahi (a.s) amesema kumwambia Abu Muhammad: “ewe Abu Muhammad, kwa hakika sisi tuna siri na elimu zitokazo kwa Mola wetu, Wa-Llahi hakuna hata mmoja anayeweza kuzihimili siri na elimu hizo, si Malaika wala Mtume aliyetumwa na wala si muumini aliyetahiniwa na kufaulu vyema mitihani ya Mola wake anayeweza kuzihimili siri na elimu hizo. Wa-Llahi hakuna aliyepewa wadhifa wa kuzihimili siri na elimu hizo zaidi yetu, wala hakuna aliyemuabudu Mola kupitia siri na elimu hizo zaidi yetu….[1] Imepokewa kutoka kwa Imamu Saadiq (a.s) akisema: “Sisi tuna elimu na siri kutoka kwa Mola wetu, siri na elimu ambazo haziwezi kubebwa na yeyote yule miongoni mwa Malaika walio karibu na Mola wao, wala Mitume waliotumwa kabla ya Mtume (s.a.w.w), wala muumini aliyetahiniwa na kupasi vyema mitihani ya Mola wake,  na hakuna hata mmoja aliyetwishwa wadhifa wa kuvihifadhi vitu viwili hivyo zaidi yetu, pia hakuna yeyote aliyemuabudu Mola wake kupitia elimu hiyo zaidi yetu”.

Kwa hiyo kama kuna utata wowote kuhusiana na ubora wa kielimu wa Maimamu, utata huo unatakiwa kuchunguzwa chini ya mlolongo wa Hadithi kama hizo. Na tegemeo la wanazuoni wa Kishia katika kuuthibitisha ubora huo limeegemea kwenye aina kama hizo za Riwaya.

Kabla ya sisi kuanza kulifanyia utafiti suala la daraja za Maimamu (a.s) zilivyo, kwanza kabisa ni lazima tuelewe kuwa: obora wa wanaadamu juu ya Malaika, ni moja kati ya mambo yasiyokuwa na ubishi mbele ya Waislamu tofauti, na baada ya kukubalika kwa suala hilo mbele ya Waislamu hao, basi sisi hatuoni kuwepo kwa tatizo muhimu, kuhusiana na ubora wa Maimamu (a.s) juu ya Malaika wa Mwenye Ezi Mungu. Hapo lililobakia kuwa ni moja kati ya masuala yanayotaka uhakiki maalumu, ni lile suala la ubora wa Maimamu hao juu ya Mitume waliopita (a.s), na jambo hili linaweza kuthibitishwa kupitia dalili tofauti za Kimantiki, na wala kulithibitisha suala hilo huwa hakusababishi kuvuruga baadhi ya misingi na itikadi za Kiislamu, bali uthibitishaji wa sulala hilo, ni jambo moja muhimu lenye uhusianao wa moja kwa moja na Uhakika kamili wa Uislamu. Pia kuutambua uhakika huo, ni moja kati ya nyadhifa za Waislamu, kwani Maimamu ndio watu waliokamilika kiutu na kiubinaadamu wanaotakiwa kutambuliwa na kila mmoja wetu. Kulithibitisha suala hilo kunahitajia kupita katika vipengele vifuatavyo:

1- Maasuumina (Watakatifu) kumi na nne, ni watu walioumbwa kupitia nuru moja, uhakika wao huo uliojengwa kupitia nuru moja, umethibitishwa ndani ya Hadithi mbali mbali, huku Hadithi hizo zikiwatakasa watu hao kupitia njia mbali mbali, na miongoni mwa Hadithi hizo, ni ile Hadithi ya wale watu watano wa kisaa (Ahlul-Kisaa), huku Hadithi nyengine zikiwatakasa wote 14 kwa ujumla kwa mtindo mmoja. Miongoni mwa Hadithi zinazowatakasa wao, ni kama ifuatavyo:

A- Mola Mtukuffu Amesema: “Ewe Muhammad, kwa hakika mimi nimekuumba wewe, pia nikamuumba Ali na Fatima na Hassan na Husein kupitia nuru yangu, kisha nikayatangaza mamlaka yenu na ubora wenu kwa wanambingu na ardhi, kwa hiyo yule atakaye yakiri mamlaka yenu, huyo nitamuhesabu kuwa ni miongoni mwa waumini, na yule atakayelipinga hilo, atahesabika kuwa ni miongoni mwa Makafiri, ewe Muhammad, lau mja miongoni mwa waja wangu ataniabudu hadi auvunje mgongo wake kwa wingi wa ibada, au awe kama mti uliokauka, kisha aje kwangu huku akiwa ni mwenye kuyakanusha mamlaka yenu, kwa kweli mimi sitamsamehe mja huyo mpaka pale atakapoyakiri mamlaka na fadhila zenu”.[2] Maneno haya yamenukuliwa kutoka kwenye Hadithi ya Mi’iraji.

B- Mola Mtukufu anamwambia Mtume wake (s.a.w.w) maneno yafuatayo: “Ewe Muhammad, kwa hakika mimi nimemuumba Ali, Fatima, Hassan na Husein pamoja na Maimamu kupitia nuru moja, kisha nikayatangaza mamlaka yao juu ya walimwengu, hivyo basi, yule atakayeliridhia suala hilo na kulikubali, atakuwa miongoni mwa waumini, na yule atakayelikanusha, atakuwa ni miongoni mwa makafiri, ewe Muhammad, lau atokee mja miongoni mwa waja wangu atakayeniabudu hadi kukatika mgongo wake kutokana na wingi wa ibada, kisha arejee kwangu huku akiwa ni mwenye kuyakusha mamlaka yao (Maimamu), huyo nitamuingiza motoni….”[3] Miongoni mwa yale yalioashiriwa ndani ya Hadithi hii, ni kule Maimamu wote kuumbwa kutokana na nuru moja.

2- Maimamu wote ni wenye mamlaka ya uongozi waliobarikiwa na Mola wao.[4]  Hii inamaanisha kuwa wao ndio wenye zamu za kushika madaraka ya kuiongoza jamii pamoja na kufutu maswali mbali mbali ya kisheria baada tu ya Mtume (s.aw.w) kufariki. Maimamu ni wenye nguvu zitokazo kwenye ulimwengu wa Ghaibu kwa ajili ya kuwaongoza walimwengu pamoja na kuyatatua matatizo mbali mbali ya jamii. Wao pia wana uwezo wa kizifahamu nyoyo za watu tofauti, pamoja na usafi wa nyoyo za watu hao ulivyo.

Mwanachuoni maarufu ajulikanaye kwa jina la Tabaatabaai (r.a) anasema: Maimau ni watu wenye mamlaka kamili juu ya matendo ya wanaadamu, kwa hiyo wao huzitumia nguvu zao kwa ajili ya kuwaongoza waja na kuwaelekeza katika njia ilio salama. Kwa lugha nyengine ni kwamba, wao wana uwezo wa kuzisarifu nyoyo za watu, kwa hiyo wao wana mamlaka ya kisheria, na pia wao wanaruhusa ya kukigeuza na kukisarifu kile wakitakacho kwa idhini ya Mola wao, kupitia mamlaka ya kuusarifu ulimwengu wa kimaumbile waliokuwa nayo.[5]

Maimamu hawana mamlaka ya kutunga sheria, na hata Mtume (s.a.w.w) hakuwa na mamlaka hayo, kwani mamlaka hayo yako kwenye mkono wa Mola Mtakatifu tu, kwa hiyo mitume pamoja na Maimamu wana wadhifa tu wa kikifikisha kile wanachoamrishwa kukifikisha bila ya kuzidisha wala kupunguza.[6],[7] Mamlaka ya Mimamu (a.s) juu ya ulimwenge huu, yanayojulikana kwa jina la (mamlaka ya kimaumbile), huwa na maana ya Wao (a.s) kuwa na mamlaka ya kukisarifu chochote kile kilichomo ndani ya ulimwengu huu kwa idhini ya Mola wao. Karama na miujiza yote inayofanywa na Mitume au Mawalii wa Mungu, huwa inatokana na ule uwezo wa kukisarifu kile wakitakacho ndani ya ulimwengu huu kupitia idhini ya Mola wao. Pia ni lazima ieleweke kuwa, kuna aina mbili za miujiza, nayo ni, miujiza ya kimatendo na miujiza ya kimatamshi.[8] Yote basi yaliyo onekana kutendwa na baadhi ya Mitume (s.a), kama vile: Kupasuka kwa mwezi,[9] na kuchanika kwa mti, kupitia Mtume Muhammad (s.a.w.w),[10] kupasuka kwa ardhi[11] na kuchanika kwa bahari[12] vilivyozungumzwa katika kisa cha Qaaruun na Firauna, kupitia kwa nabii Musa (a.s), kupasuka kwa mlima[13] kupitia kwa nabii saleh (a.s), kuwaponyesha vipofu na wenye ubalanga pamona na kuwafufua wafu, kupitia kwa nabii Isa (a.s),[14] pia kuung’oa mlango wa ngome ya Khaibar, kupitia kwa Ali bin Abi Talib,[15] matokeo yote hayo tuliyoyataja, si chengine chochote kile zaidi ya zile nguvu za mamlaka ya kuvisarifu vitu vya ulimwengu huu kupitia idhini ya Mola wao.

3- Mamlaka maalumu ya uongozi au ya kusarifu vitu vilivyomo ulimwenguni, hayapatikani ila pale mja anapoisabilia nafsi yake kikamilifu kabisa kwa ajili ya Mola wake, jambo ambalo humfanya yeye pale macho yake yanapo anguka kwenye moja kati ya vioo vya dunia, awe yeye haoni kwenye kioo hicho ila sifa za Mola wake.[16] Mja anapoisabilia nafsi yake kwa ajili ya Mola wake, yeye huwa ni mja aliyezama ndani ya bahari kubwa ya sifa kamilifu za Mola wake, na hilo humfanya yeye aipoteze nafsi yake katika bahari hiyo, kwani nafsi yake ni moja kati ya matonyo yaliyotokana na maji ya nuru ya bahari hiyo, na pale nafsi yake ambayo ni tonyo la nuru ya maji hayo linapochanganyika na bahari hiyo! Huwa si kazi rahisi ya yeye kuweza kuiona tena nafsi hiyo ndani ya bahari kama hiyo. Mja anapoungana na maji ya bahari hiyo, matendo na amali zake zote huwa na rangi ya maji hayo, yaani ingawaje mja hawezi kubadilika akawa Mungu! Lakini anaweza kubadilika akawa na sifa zenye rangi ya sifa za Mungu. Kila pale mja anapomkaribia Mola wake zaidi, ndipo anapozichana pazia za viza vya mausiku ya ujinga, na kuingia katika nuru, na kila anapokwenda zaidi ndani ya nuru hiyo, ndipo anapo potewa na nafsi yake, na hatimae kuto jiona kabisa, na kila pale anapokuwa mbali na nafsi yake ndipo sifa za Mola wake zinapoivaa nafsi yake, na kila sifa za nafsi yake zinapokolea rangi ya sifa za Mola wake ndipo matendo yake yanapoendana na matakwa ya Mola wake.[17] Hii ni kwa kutokana na kwamba, kudra za Mwenye Ezi Mungu ni jambo lisilo na mipaka, hivyo basi pale mja anapoungana na bahari ya Mola wake, naye hupata rangi ya kudra hiyo, lakini mja huyo huwa haitumii kudra na uwezo aliokuwa nao kinyume na amri za Mola wake, kwa hiyo yeye hutenda baadhi ya vitendo kupitia uwezo huo kwa idhini ya Mola wake, na si kupitia matakwa ya nafsi yake.

Kuna Hadithi moja iliyopokelewa kutoka kwa Mola Mtakatifu, isemayo: “Ewe mja wangu hebu chunga haki zangu ili nikuveke sifa zangu,[18] ewe mwana wa Adamu, kwa kweli mimi ni tajiri nisiye fukarika, basi zitii amri zangu, ili nikufanye uwe si mhitaji wa wengine, ewe mja wangu, mimi ni mwenye uhai wa milele, basi zitii amri zangu ili nikupe uhai wa milele, ewe mja wangu mimi hukiamrisha kitu nikitakacho kiwe na papo hapo huwa, kama vile nilivyo kiamrisha kiwe, basi nitii mimi ili nikupe uwezo wa kukiambia kitu kiwe vile utakavyo wewe.[19]

4- Daraja ya Uimamu inatofautiana sana na daraja ya Utume, kwani daraja ya Uimamu ni cheo maalumu chenye daraja ya juu zaidi ya cheo cha Utume. Pale walii wa Mungu anapoiingia bahari ya sifa za Mola wake, hapo hufunukiwa na kupata elimu ya inayofungamana moja kwa moja na uhakika wa Mola wake, na pale anapokuwa tayari ameshapikika kiasawasawa na kupata ufunuo wa Mola wake, hapo yeye hutoa habari alizozipata kutoka Ughaibuni na kuwafikishia wengine kwa jinsi ya matakwa ya Mola wake yalivyo, hapa Mawalii wa Mola wanaweza kupata aina zote mbili, au aina moja tu kati ya vyeo vifuatavyo:

A- Unabii: Walii anaweza kupewa cheo cha Unabii bila kupata cheo cha Utume. Unabii una maana ya kwamba: yeye tayari amefikia cheo cha kupokea Wahyi kutoka kwa Mola wake, lakini bado yeye hana ruhusa ya kuutangaza Wahyi huo kwa wengine, na wakati mwengine, walii huwa anapokea Wahyi kutoka kwa Mola wake, lakini Wahyi huo huwa ni kwa ajili yake yeye tu, na si kwa ajili ya watu wa jamii yake. Pia imesemwa kuwa Nabii huwa hana kitabu alichoteremshiwa kwa ajili ya sheria, bali yeye hufuata kitabu cha mtume aliyetumwa kabla yake au cha yule mtume anayeishi ndani ya zama zake.

B- Utume: Utume una maana ya pale Walii wa Mwenye Ezi Mungu kupata ruhusa ya kuutangaza Wahyi wa Mola wake kwa wengine, kwa ibara nyengine ni kwamba: Utume ni ile hali ya Walii kuteuliwa kwa ajili ya kuwafikishia wengine Wahyi pamoja na amri maalumu kutoka kwa Mola wao.

Hivyo basi Mtume huwa hawezi kuwa ni Mtume bila ya kukifikia cheo cha Unabii, kwani maana ya Unabii ni kule mja kukifikia cheo cha kupokea Wahyi kutoka kwa Mola wake. Na hii ina maana ya kwamba kila Mtume ni Nabii, lakini sio kila Nabii ni Mtume.

Mwenye Ezi Mungu katika Qur-ani anamzungumzia Nabii Yusuf (a.s) kwa kusema: “Na pale yeye alipofikia Baleghe na kutimia kisawa sawa, Sisi tukampa sheria na elimu, na hivyo ndivyo tunavyowalipa wale waliozama katika bahari ya sifa za Ihsani”.[20] Kinachotakiwa kuzingatiwa kutokana na maelezo haya, ni kwamba: sisi hatuwezi kupata cheo cha Utume, kwani viti vya cheo hicho, tayari vimeshakamilika na walio na mamlaka ya kuvikalia viti hivyo pia wameshatambulikana na wameshakamilika. Lakini bado kuna nafasi nyingi za kuifikia daraja ya Uwalii, daraja ambayo huwa na mamlaka ya mja kukitenda kile akitakacho kwa amri tu, bila ya yeye mwenyewe kupata tabu, lakini ni lazima tufahamu kuwa: iwapo mja atamuabudu Mola wake kwa nia ya kupata mamlaka maalumu, huyo atakuwa hana haja na Mola wake, bali haja yake itakuwa ni kuyafikia hayo malengo yake ya kupata mamlaka maalumu.

Tofauti baina ya cheo cha Uimamu (Uwalii maalumu) na Utume:

Kuna baadhi ya mambo maalumu yanayo vitofautisha vyeo viwili hivi, na baadhi ya mambo hayo ni kama ifuatavyo:

1- Kinachozingatiwa katika chanzo cha cheo cha Uwalii au Uimamu ni ule uhakika wa johari asili ya cheo hicho, ama kianachozingatiwa katika Utume ni ile hali ya dhahiri ya ufikishaji au utowaji habari za Ghaibu, jambo ambalo huwa linatokana na ile chemchem ya uhakika asili wa johari ya Uwalii.

2- Mitume kutokana na kuwa wao wamezama kisawa sawa kwenye bahari ya Upweke wa Mola wao, hilo huwa linawawezesha wao kuona aina mbali mbali za siri za Ughaibuni, na wakati mwengine kuzifikisha habari hizo kwa waja wengine, lakini tusisahau kuwa chimbuko la cheo chao, ni ule uhakika wa johari yao iliyo ungana na nuru ya Mola wao iliyowapa wao cheo hicho cha Uwalii wenye mamlaka maalumu tuliyoyaelezea hapo mwanzo.

3- Walii huwa ni mjuzi wa sheria pamoja na aina Mbali mbali za uhahika dhahiri wa mambo pamoja na undani wake, Yeye hua ana elimu ya dhahiri na batini (uhakika halisi) yenye kumfunulia uhakika halisi wa mambo yalivyo. Ama kazi za mitume, huwa zinazingatia udhahiri wa lile suala la wao kuwa na aina maalumu ya sheria walioamriswa kuifikisha kwa waja.

4- Walii huwa anaujuwa uhakika wa nafsi ya kila mmoja, hivyo basi kuwatii wao huwa ni wajibu wa kila mmoja wetu.

5- Nabii na Rasuli,huwa wanapata elimu zao kupitia Malaika maalumu, lakini Walii (Maimamu) huelimika kupitia njia ya ndani kwa ndani iliyoungana na uhakika wa nuru ya Mtume (s.a.w.w), na hatimae kuungana na nuru ya Mola Mtakatifu.[21]

6- Uhakika wa Uwalii, umebeba ndani yake aina zote za vyeo vya Utume, Unabii wenye jukumu la kuitangaza na kuilinda sheria, pamoja na Unabii binafsi wenye elimu na siri maalumu kwa ajili ya kumuabudu Mola wao, jambo ambalo huwa ni siri baina yao na Mola wao.

7- Uhakika wa Utume na Unabii, unatokana na ni ile rangi ya nje ya Uhakika wa nuru ya johari ya Mola, ama uhakika wa Uwalii (Uimamu), unatokana na ule uhakika wa ndani wa nuru ya johari ya Mola Mtakatifu.

8- Asili ya Unabii na Utume inatokana na johari ya Uwalii (Uimamu), kwa hiyo Utume na Unabii unahitajia msigi wa Uwalii kwa ajili ya kilijenga jengo la Utume au Unabii juu yake.[22]

Natija ya utafiti

Utafiti tulioufanya ndani ya malaka hii, umeweza kutufunulia ufukwe mpya kapisa wa utambuzi juu ya tofauti zilizopo baina ya cheo cha Uwalii (Uimamu), Utume pamoja na unabii. Baada ya utafiti huu kukamilika na kulikunja pazia lake, sisi tumeonekana kuyafahamu mambo yafuatayo:

A- Cheo cha Uwalii (Uimamu) wa mtume fulani, huwa ni chenye daraja kubwa zaidi ya cheo cha utume wake.

B- Yawezekana mtu akapata Uwalii, bila ya yeye kuwa ni mtume, lakini yeye kutokuwa na cheo cha utume huwa hakumaanishi kuwa yeye ni wenye hadhi ya chini, bali yawezekana yeye akamzidi mtume kidaraja, jambo ambalo huwa linatokana na hadhi ya daraja ya Uwalii aliyonayo pamoja na elimu yake ilivyo. Na hilo ndilo linalo onekana katikaa kile kisa cha Nabii Musa na Hidhri (a.s), Hidhri alimwambia wazi wazi Nabii Musa (a.s) ya kuwa yeye (Musa) hutokuwa na subira endapo atafanya usihaba na Hidhri (a.s), aliendelea kumwambia Musa (a.s) ya kuwa “Ewe  Musa we! vipi wewe utaweza kuwa na subra juu ya yale uliokuwa huna elimu nayo? Na baada ya Musa (a.s) kumshikilia sana katika kumuomba Hidhri usahiba, mwishowe Hidhri akakubali kufuatana naye katika safari yake, lakini kwa kutokana na elimu ya Musa kuwa ni ndogo kuliko ya Hidhri, yeye akawa ameshindwa kuvumilia, na hali ikawa ndiyo ile ile iliyokadiriwa na Hidhri kutokea, nayo ni ile hali ya Musa kutokuwa na subra.[23] Na hilo ndilo litakalomfanya Nabii Isa (a.s) kukaa nyuma ya Imamu Mahdi (a.s) pale Yeye atapodhihiri, ingawaje Isa (a.s) ni miongoni mwa mitume wenye cheo cha Ulul-Azmi, lakini yeye ataonekana kukaa nyuma ya Imamu Mahdi (a.s).[24] Kwa lugha rahisi zaidi ni kwamba: ingawaje walii Hidhri pamoja na Imamu Mahdi (a.s) si miongoni mwa wale walioteremshiwa kitabu cha sheria, lakini tumeona wazi kuwa Hidhri alimzidi Musa (a.s) kielimu na kidaraja, kama vile Imamu Mahdi (a.s) alivyomzidi Isa (a.s). Usemi wa imamu Ali (a.s) pia ni wenye kulitilia mkazo suala hilo pale yeye aliposema: “Kwa hakika mimi ninaiona nuru ya Wahyi na Ujembe wake, pia ninaisikia harufu ya Utume, na kwa hakika mimi nimeusikia mguno wa Shetani pale Wahyi ulipokuwa ukiteremka”. Pia Mtume (s.a.w.w) alimwambia Ali bin abi Taalib maneno yafuatayo: “Ewe Ali, kwa hakika wewe unayasikia yale ninayoyasikia na unayaona yale ninayoyaona, kwa hiyo tofauti baina yangu mimi na wewe, ni kule tu kuwa wewe si mtume”.[25] Imamu Hassana baada ya kufariki Ali bin Abi Taalib, alisema kuwambia watu: “Enyi watu, kwa hakika ndani ya usiku wa leo amefariki yule ambaye hakutokea mtu hata mmoja wa kumzidi yeye kidaraja, si katika watu waliotangulia wala wale watakao kuja baada yake, ila tu yeye hakuwa na cheo cha utume”.[26] Na Mtume (s.a.w.w) katika Riwaya nyengine amesema: “Kwa hakika Mola ana waja walio karibu naye zaidi kuliko mitume, na wala wao si miongoni mwa mitume, bali hata mtume wenyewe wanatamani lau wangeweza kuzifikia daraja hizo za ukaribu wa Mola wao walizo nazo waja hao”.[27] Hadithi hii imeeleza wazi suala la baadhi ya waja kuwapindukia mitume kidaraja, na pia sababu ya wao kupata daraja hizo imefafanuliwa na Hadithi hii, na sababu yenyewe, ni kule kuwa wao wako karibu zaidi na Mola wao.

Mola mtukufu katika Qur-ani Anasema: “Na wale waliokufuru wanasema: kuwa wewe si mjumbe wa Mola, basi waambie: yatosha kuwa Mola ndiye shahidi baina yangu mimi na nyinyi, na pia yule ambaye elimu ya kitabu iko kwake (ni shahidi baina yetu)”.[28] Ndani ya Ayah hii, Mola ameleta mashadi wawili kwa ajili ya kuuthibitisha Utume wa Mtume wake (s.a.w.w), shahidi wa kwanza ni Yeye mwenyewe (s.w), na shahidi wa pili ni yule ambaye elimu ya kitabu iko kwake. Mwenye Ezi Mungu hulithibitisha alitakalo kupitia miujiza yake, na moja kati ya miujiza hiyo, ni Qur-ani Tukufu, ni nini basi kinachotumiwa na yule ambaye elimu ya kitabu iko kwake, katika kuuthibitisha ukweli wa Mola Mtukufu? Na ni nani huyo aliyetajwa kuwa elimu ya kitabu iko kwake? Bila ya kusita sisi tunatoa jawabu kwa kusema: yule ambaye elimu ya kitabu iko kwake, ni Imamu Ali pamoja na Maimamu waliotoharika (a.s), kwani wao ndiwo wenye daraja ya Uwalii wenye mamlaka ya kuusarifu ulimwengu na vile vilivyomo ndani yake kwa idhini ya Mola wao.

Ili suala hili lieleweke vizuri zaidi, hebu basi tukiangalie kisa cha Nabii Suleimaan (a.s) na yule mfalme wa Saba-a aliyejulikana kwa jina la (Bilqiis) kilivyokuwa, kwani kisa hichi kinaweza kuwa ni msaada mzuri wa kulifahamu suala letu hili, kisa hichi kinaanza kwa kusema: Hud-hud[29] alipaa na kufunga safari ya kuelekea mji wa (Saba-a), na pale aliporudi almpa habari Nabii Seleimaan (a.s), zisemazo kuwa: “mji wa Saba-a ni wenye kumilikiwa na mfalme wa kike aliyejulikana kwa jina la Bilqiis, naye ni mwanamke mwenye ufakhari wa hali ya juu, kwani yeye anamiliki kila kitu kwa ajili ya mahitajio yake, naye ni mwenye kiti kikuu cha ufalme chenye kupendeza! Watu wa mji huo ni wenye kuabudu jua badala ya kumuabudu Mola wao”! Nabii Suleimaan akaamua kumuandikia barua mfale huyo, huku akimtaka yeye na wafuasi wake waje kwake hali wakiwa wamesalimu amri na kuikubali haki. Pale mfalme alipoisoma barua ile akaamua kumtumia zawadi Nabii Suleimaan (a.s), ili iwe ni kama hongo. Suleimaan (a.s) alizikaa zawadi hizo, kisha akawambai wafuasi wake: “Enyi wakuu, ni nani atakayeniletea kiti cha ufalme cha mfale wa Saba-a, kabla ya yeye kuja hapa hali akiwa amesalimu amri? Mmoja kati ya Maafiriti wa kijini alisema: “mimi nitakuletea kiti chake kabla ya wewe kuondoka katika kikao ulichokaa, nami kwa hilo tu, ni mwenye uwezo kamili”, miongoni mwao alikuwepo mtu aliyekuwa na elimu ya kitabu, naye alisema kumwambia Nabii Suleimaan: “mimi nitakuletea kiti chake kabla ya hata jicho lako kurudi kutoka mawesoni mwake!” basi pale Nabii Suleimaan alipokiona kile kitiki kiko mbele yake alisema: “Kwa kweli hizi ni miongoni mwa fadhila za Mola wangu”.[30]

Katika kisa hichi sisi tumeona jinsi ya yule aliyekuwa na elimu ya kitabu alivvyofanya makarama yake, yeye kufumba na kufumbua alikileta kiti cha mfalme Bilqiis kutoka Yemen kwenda Palestina, yeye alifanya hivyo kupitia yale mamlaka ya kukisarifu akitakacho, kwani yeye alikuwa ni miongoni mwa Mawalii wa Mola, kwa ibara nyengine zilizokuja kwenye baadhi ya Hadithi, ni kuwa yeye alilitumia jina kuu la mwenye Ezi Mungu katika kukileta kiti hicho, jina ambalo huitwa kwa kwa lugha ya Kiarabu  (  .(اسم الله الاعظم

Walii huyu aliyefainya kazi ya kukileta kile kiti, alikuwa akimiliki baadhi tu ya elimu ya kitabu na wala sio elimu yote ya kitabu, na ibara ya Qr-ani imemuelezea yeye kwa kusema:

 (قالَ الَّذي عِنْدَهُ عِلْمٌ مِنَ الْكِتابِ أَنَا آتيكَ بِهِ قَبْلَ أَنْ يَرْتَدَّ إِلَيْكَ طَرْفُكَ), yaani (akasema yule mwenye elimu kutoka kitabuni: mimi nitakuletea kiti hicho kabla ya kufumba na kufumbua). Mtume (s.a.w.w) akimwambia Abu-Said Al-khudriy kuhusiana na Walii huyu alisema: “aliyekusudiwa ndani ya Aya hiyo, alikuwa ni Wasii wa ndugu yangu Nabii Suleimaan bin Daud ambaye alikuwa akiitwa (Aasif bin Barkhia) naye ni mtoto wa dada yake (Nabii Suleimaan), na maana ya kauli (وَ مَنْ عِنْدَهُ عِلْمُ الْكِتابِ) (pale iliposemwa: “Na wale waliokufuru wanasema: wewe si mjumbe wa Mola, basi waambie: yatosha kuwa Mola ndiye shahidi baina yangu mimi na nyinyi, na pia yule ambaye elimu ya kitabu iko kwake (ni shahidi baina yetu)[31], ni ndugu yangu Ali bin Abi Taalib”.[32]

 Ni jambo la wazi kuwa, kuna tofauti kubwa baina ya: «مَنْ عِنْدَهُ عِلْمُ الْكِتابِ»  na «قالَ الَّذي عِنْدَهُ عِلْمٌ مِنَ الْكِتابِ» kwani Aya mwanzo ina maana isemayo: (Akasema yule ambaye ana elimu kutoka kitabuni), yaani yeye ana baadhi tu ya elimu ya kitabu, huku Aya ya pili ikiwa na maana isemayo: (yule ambaye elimu ya kitabu iko kwake), yenye maana ya kwamba elimu ya kitabu yote iko kwake.[33] Imamu Saadiq (a.s) aliisoma Aya Isemayo:

 «قالَ الَّذي عِنْدَهُ عِلْمٌ مِنَ الْكِتابِ» kisha akasema: «وَ عِنْدَنَا وَ اللَّهِ عِلْمُ الْكِتَابِ كُلُّهُ», yaani (Naapa kwa jina na Mola ya kwamba elimu yoye ya kitabu iko kwetu sisi).[34] Bayana zilizipita zimetupa ufumbuzi wa kutambua kuwa, Mawalii ni wenye kutofautiana kidaraja na kielimu, kwa hiyo yaweza mmoja akawa na uwezo wa kutenda jambo kwa kufumba na kufumbua, huku mwengine akahitajia muda zaidi katika kutenda matendo yake ya makarama, kama tulivyoona katika kisa kilichopita.

Mwisho tunawausia wale wenye shauku zaidi ya kufanya utafiti zaidi juu ya mada hii, kurudia kitabu cha Kipashia kiitwacho: Negareshe Irfaniy Falsafiy wa Kalaamiy be shakhsiyyate wa qiyaame Imamu Husein (a.s).[35]

 


[1] Alkafi cha Thiqatul-Islam Koleiniy, juz/1, uk/402, chapa ya Daarul-Kutubil-Islamiyya, Tehran.

[2] Bihaarul-Anwaar, cha Muhammad Baaqir Majlisiy, juz/36, uk/216.

[3] Rejeo iliyopita, uk/281 hadi 223.

[4] Imamu Ali akiashiria suala hilo alisema:   «وَ لَهُمْ خَصَائِصُ حَقِّ الْوِلَايَة»؛  “Nao (Maimamu) wa sifa ya mamalaka ya uongozi”. Rejea hutuba ya pili ya kitabu (Nahjul-Balagha ).

[5] Al-miizaan, cha Muhammad Husein Tabaatabaai, juz/1, uk/275 hadi 276.

[6] Kuna kauli zisemazo kuwa: Mola Mtukufu amempa Mtume (s.a.w.w) mamlaka ya kuweza kuongeza baadhi ya mambo fulani katika sheria, Naye (s.a.w.w) aliitumia nafasi hiyo kwa kuongeza baadhi ya sheria fulani, na miongoni mwa vitu alivyoviongeza Mtume (s.a.w.w), ni rakaa ya tatu naya nne za sala ya Adhuhuri na Al-Asiri. Ikiwa jambo hilo litathibiti, basi halitoweza kuthibiti kwa Mitume wengine walio bakia pamoja na Maimamu, bali jambo hilo litakuwa ni zawadi maalumu kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) peke yake.

[7] Suratul-Jaathia Aya ya 19. Suratu Shura Aya ya 13 na 22. Suratu Ra’ad Aya ya 8. Suratu Israa Aya ya 106. Pia rejea kitabu (Al-Futuuhaat) cha Ibnu Arabiy, juz/4, uk/69.

[8] Miujiza ya kimaneno ni yenye kukusanya zile kauli za Mtume na Maimamu zilizobeba maana nzito kutoka kwa Mola wao, maneno ambayo ni yenye kumshangaza kila mwenye akili,  tofauti baina ya muujiza wa maneno na muujiza wa vitendo, ni kuwa: muujiza wa vitendo ni muujiza wenye kwenda na wakati ndani maisha ya mwenye muujiza huo, ama muujiza wa maneno ni wenye kubaki milele hata kama mwenye maneno hayo atakuwa tayari ameshafariki.

[9] Moja kati ya miujiza ya kimatendo ya Mtume (s.a.w.w), ni kupasuka kwa mwezi.

[10] Kumeonekana katika kitabu (Nahjul-Balagha) maneno ya Imamu Ali (a.s) akizungumzia muujiza wa kupasuka kwa mti.

[11] Suratul-Qasas Aya ya 76 hadi 81.

[12] Suratul-Baqara Aya ya 50.

[13] Suratush-Shamsi, Aya ya 11 hasi 15.

[14] Suratu Aali-Imraan, Aya ya 49.

[15] Imamu ali (a.s) aliliashiria hilo katika barua yake kwa Othman bin Haniif akisema:

«وَ اللَّهِ مَا قَلَعْتُ بَابَ خَيْبَرَ وَ رَمَيْتُ بِهِ خَلْفَ ظَهْرِي أَرْبَعِينَ ذِرَاعاً بِقُوَّةٍ جَسَدِيَّةٍ وَ لَا حَرَكَةٍ غِذَائِيَّةٍ لَكِنِّي أُيِّدْتُ بِقُوَّةٍ مَلَكُوتِيَّةٍ وَ نَفْسٍ بِنُورِ رَبِّهَا مُضِيئَة»

“Mimi sikuung’oa mlango wa Khaibar kwa nguvu za kiwiliwili, au kwa kutokana na nguvu za shibe ya mwili wangu, bali niliung’oa huku nikisaidiwa na nguvu za Ghaibu, kwani nafsi yang’aa kwa nuru ya Mola wake”. Rejea majlisi ya 77, uk/513.

[16] Kuna aina mbili za kuisabilia nafsi na kuzama kwenye bahari ya Mola: ya  kwanza ni mtu kuzama katika bahari hiyo kimatendo, kiasi ya kwamba akawa yeye hatendi lile alitakalo bali atenda lile alitakalo Mola wake, na ya pili, ni kuzama kwa nafsi na dhati ya mja huyo katika bahari hiyo. Rejea kitabu (Ishaaraat-wa-tanbiihaat) cha Ibnu Sina, kilichoshereheshwa na Khooja Nasiirud-Diiin Tuusiy, juz/3, maqaamaatul-aarifiin  uk/390. Pia kitabu cha Hadithi 40 cha Imamu Khomeiny, uk/382.

[17] Imamu Mujtaba (a.s) amesema: “Mwenye kumuabudu Mola wake,  Mwenye Ezi Mungu huvitiisha vitu vyote na kuviweka kwenye mamlaka yake kwa ajili ya huduma yake”. Tafisiri yenye kunasibishwa na Imamu Askari (a.s), juz/1, uk/327. Bihaarul-Anwaar, cha Muhammad Baaqir Majlisiy, juz/68, uk/184.

[18] Andiko la Hadithi hii lipokewa kwa lugha ya Kiarabu kama ifuatavyo: «عبدی اطعنی حتی اجعلک مثلی...» Rejea kitabu (Asraaru-salaati), cha Mirza Jawadi Aghaa Tabriiziy, juz/1, uk/4 katika utanguli wa kitabu hicho. Sherhe Duaai Sabaah cha Molla Mustafa Khuui, juz/1, uk/11. Jaamiul-Asraar-wa-manba’al-anwaar, cha Sayyid Haidar Aamuuliy, uk/363.

[19] Andiko kamili la Riwaya hii ni kama ifuatavyo:

«ابن آدم أنا غني لا أفتقر أطعني فيما أمرتك أجعلك غنيا لا تفتقر يا ابن آدم أنا حي لا أموت أطعني فيما أمرتك أجعلك حيا لا تموت يا ابن آدم أنا أقول للشي‏ء كن فيكون، أطعني فيما أمرتك أجعلك تقول لشي‏ء كن فيكون»

Rejea Bihaarul-Anwaar cha Muhammad Baaqir Majalisiy, juz/90, uk/376. Irshadil-Quluub-ila-sawaabi, cha Hassana bin Abil-Hassan Deilamiy, juz/1, uk/75. Iddatud-Daai cha Jamaalud-Diin Ahamd ibnu Muhammad ibnu Fahad Hilliy, uk/310.

[20] Suratu Yusuf, Aya ya 22.

[21] Falsafeye Irfan, cha Yahya Yathribiy, uk/181.

[22] Insane-Kaamil-az-diidgahe-Nahjul-Balaghe, cha Hassan Hassan Zade Aamuliy, uk/84 hadi 86.

[23] Suratul-Kahfi Aya ya 64 hadi 78.

[24] Bihaarul-Anwaar cha Muhammad Baaqir Majlisiy, juz/9, uk/195. Tafsiru Nemune ya Nasir Makaarim Shiraziy, juz/4, uk/205. Makhaazin cha sayyid Abbaas Kaashaaniy, juz/4, uk/286.

[25] Nahjul-Balagha, hutuba ya 192.

[26] Muruujidh-Dhahab, ch Mas-uudiy, juz/2, uk/414.

[27] Musnad Ahmad, cha Ahmad bin Hambal, juz/5, uk/343. Riyaadhus-Saalikiin, cha Sayyid Ali Khaan Madaniy Kabiir, juz/6, uk/393. Sher-he Asmaaul-Husnaa, cha Mola Haadi Sabzewaariy, uk/552. Al-Futuuhaat, cha Muhyid-Diin Ibnu Arabiy, juz/13, uk/137.

[28] Suratu Ra’adi, Aya ya 43.

[29] Hud-hud ni aina maalumu ya ndege aliyekuwa akimtumikia Nabii Suleimaan (a.s).

[30] Suratun-Namli, Aya ya 20 hadi 41.

[31] Suratu Ra’adi, Aya ya 43.

[32] Hadithi hii imepata sindikizo kutoka kwenye vitabu vya Kisunni, kwa ajili ya utafiti zaidi rejea kitabu (Ihqaaqul-Haqqi) cha Qadhi Nuru-Llahi Shoshtariy, juz/3, uk/280 hadi 281.

[33] Tafsiri Nemune ya AyatuLlahi Nasir Maarim Shiraziy, juz/15, uk/473.

[34] Al-Kaafi, cha Muhammad bin Ya’aquub Koleiniy, juz/1, uk/229.

[35] Negareshe Irfaniy Falsafiy wa Kalaamiy be shakhsiyyate wa qiyaame Imamu Husein (a.s), cha Qasim Turkhaan, chapa ya Chelcheragh.

 

TARJAMA YA JAWABU KATIKA LUGHA NYENGINE
MAONI
Idadi ya maoni 0
Tafadhali ingiza thamani
mfano : Yourname@YourDomane.ext
Tafadhali ingiza thamani
<< Niburute.
Tafadhali ingiza kiasi sahihi ya usalama Kanuni

MPANGILIO WA KIMAUDHUI

MASWALI KIHOLELA

YALIYOSOMWA ZAIDI