Please Wait
9784
Suala la ndoa ya Imamu Husein (a.s) na bibi Shahre Baanu aliyetekwa na jeshi la Kiisalamu, ni suala liliozungumziwa na vitabu vya historia huku likiwa na rangi mbali mbali za Ibara zenye kutofautiana, baadhi ya kauli zimesema kuwa: yeye alitekwa katika zama za utawala wa Omar, huku baadhi yake zikisema kuwa yeye alitekwa katika zama za utawala wa Othman. Vile vile yeye alirikodiwa na vitabu hivyo huku jina lake na la baba yeke likionekana kubadilika kutoka kitabu kimoja kwenda chengine au kutoka riwaya moja kwenda nyengine. Kwa kweli si jambo rahisi kuweza kutoa kauli ya moj kwa moja ya kuwa yeye alikuwa ni muirani au pia kusema kuwa jina lake lilikuwa ni (Shahre-Baanu), na kwa kutokana na utata huo kuhusiana na jina lake na baba yake pamoja na asili yake, hivyo basi sisi hatutoweza kutoa hukumu isemayo kuwa yeye alikuwa ni mke wa Imamu Husein (a.s) na pia ni mama wa Imamu Sajjadi (a.s).
Suala la Imamu Husein (a.s) kumuoa binti wa Kiirani aitwae Yazdgerd, ni suala lenye utata katika uwanja wa tarehe, na kuna kauli mbali mbali kuhusiana na tokeo hilo, miongoni mwa kwauli hizo ni kama ifuatavyo:
1- Sheikh Saduuq alipokuwa akimzungumzia mama wa Imamu Zeinul-Abidiin (a.s), amenukuu Hadithi kutoka kwa Sahli bin Qasim isemayo: mimi (Sahili bin Qasim) nilipokuwa katika mji wa Khurasani Imamu Ridha (a.s) aliniambia hivi: “sisi tuna uhusiano wa kifamilia na nyinyi (Wairani)” hapo nikamuuliza: uhusiano huo umepatikana vipi? Yeye akanijibu kwa kusema: “pale Abdu-Llahi bin Kuraiz alipouvamia mji wa Khurasani, aliwachukuwa mabinti wawili wa mfalme Yazdgar wakiwa ni kama mateka na hatimae kuwapeleka kwa khalifa Othaman bin Affaan. Othaman alimcukuwa mmoja miongoni mwao na kumtunukia Imam Hassan (a.s), na wa pili akamtunukia Imamu Husein (a.s), mabinti hao wawili walifariki dunia baada ya kujifungua. Yule binti aliye olewa na Imamu Husein (a.s) akamzaa Imamu Sajjaad (a.s) na baada ya kufariki binti huyo, Imamu Sajjaad (a.s) akalelewa na mmoja kati ya watumishi wa kike wa Imamu Husein (a.s).[1] Kwa misingi ya Riwaya hii ni kwamba: binti wa Yazdgerd alipelekwa Madina katika zama za Othman na sio katika zama za utawala wa Omar bin Khattaab.
Sheikh Abbaas Qummiy anasema kuwa Riwaya hii ni yenye kutofautiana na Riwaya mbali mbali zilizoeleza kuwa binti huyo alipelekwa Madina katika zama za utawala wa Omar bin Khattaab, na Riwaya hizo ni zenye kipau mbele zaidi kuliko hiyo Riwaya ya mwanzo.[2]
2- Sheikh Koleiny (r.a) akiufafanua utambulisho wa mama yake Imamu Sajjaad (a.s), alinukuu Hadithi ifuatayo: “Pale binti wa Yazdgerd alipofikishwa mbele ya Omar, wasichana wa Madina wakalizongea eneo hilo kwa shauku ya kumuona binti huyo, na pale alipofikishwa msikitini, watu wakajaa humo kwa ajili ya kumuona, Omar hakuhuzunishwa na hali ya ugeni uliomvaa binti huyo, hapo binti huyo ajajitupia mtandio wake vizuri huku akisema: “laana imuendee Hormoz (aliyenifanya mimi kuwepo hapa)”! Omar akamgeukia na kusema: “muangalieni anavyonitukana”! Ali bin Abi Talib (a.s) akamuambia Omar: “wewe huna haki ya kumdhuru yeye, bali unatakiwa kumpa uhuru wa kumchagua amtakaye miongoni mwa Waislamu waliopo hapa.” Omar akamwachia amchague mtu amtakaye. Msichana akauweka mkono wake juu ya kichwa cha Imamu Husein (a.s). Ali (a.s) akamuuliza yule msichana kwa kumwambia: “wewe unaitwa nani?” akamjibu: “ninaitwa Jihanshaa” Ali (a.s) akamwambia: “bali wewe ni Shahre-Baanu”. Na baada ya Imamu Ali (a.s) kusema hayo alimuelekea Imamu Husein (a.s) na kumwambia: “ewe Aba Abdi-Llahi! Binti huyu atakuzaliya kiumbe bora juu ya ardhi hii”, na binti huyu akamzaa Ali bin Husein (a.s). Ali bin Husein (a.s) aliitwa mwana wa teule mbili, huku neno hilo likimaanisha kuwa baba yake ametokana na uteule wa Mola juu ya utume wa baba yake Muhammad (s.a.w.w), na kwa upande mwengine Mola akamteuwa mama yake kutoka Irani na kumuingiza katika Uislamu na kumuweka ubavuni mwa mjukuu wa Mtume Wake (s.a.w.w).[3]
Riwaya hii imetiwa mashaka na utata na wahakiki mbali mbali, na moja kati ya yaliyosemwa kuhusiana na Riwaya hiyo ni kuwa: mapokezi ya Riwaya hiyo ni yenye mashaka, kwani miongoni mwa wapokezi wake ni Amru bin Shimri, naye ni miongoni mwa wapokezi wasiosadikiwa kuwa na sifa kamili za uaminifu katika chungio ya elimu inayohusiana uchunguzi juu ya wapokezi wa Riwaya mbali mbali, ujulikanayo kwa Kiarabu kwa jina la Elmur-Rijaali.[4] Pia Riwa hii imetiwa mashaka kutokana na maandiko yake, na miongoni wa maandiko yenye utata ndani yake ni:
A- Kutekwa binti wa mfalme Yazdgerd ni suala lenye utata ndani yake.
B- Imamu Husein (a.s) kumuoa binti huyo katika zama hizo ni jambo linalotiliwa mashaka, kwani Riwaya ya kwanza imenukuu kuwa tokeo hilo lilitokea mwaka wa 22 Hijiria katika zama za utawala wa Othamani, huku Riwaya ya pili ikkilinukuu tokeo hilo kutokea katika zama za Omar, jambo ambalo haliwiyani na umri wa Imamu Husein (a.s), kwani kuvamiwa kwa utawala wa Wairani kulitokea katika mwaka wa pili wa ukhalifa wa Omar, huku Imamu Husein (a.s) akiwa na kiasi cha miaka 10 hadi 11 tu, umri ambao mtu huwa bado hajawa tayari kubeba jukumu la kifamilia (kuoa).
C- Kuhusiana na nasaba ya mama wa Imamu Sajjaad (a.s), ni jambo lenye utata pia mbele ya wanatarehe, huku baadhi yao wakiwafikiana kuhusiana na jina la mama huyo, na kutofautiana mitazamo kuhusiana na nasaba yake. Wanatarehe kama vile: Yaa’qubiy aliyefariki mwaka 284 Hijiria,[5] Muhammad bin Hasan Qummiy,[6] Koleiniy aliyefariki mwaka 329 Hijiria,[7] Muhammad bin Hasan Saffaar Qummiy aliyefariki mwaka 290 Hijiria, ambaye umaarufu wake ni Allaama Majlisiy,[8] Sheikh Saduuq aliyefariki mwaka 381 Hijiria,[9] Sheikh Mufiid aliyefariki mwaka 413 Hijiria,[10] wote hao wamekubaliana kuhusiana na mama huyo kuwa yeye alikuwa ni binti wa mfalme Yazdgerd, lakini wao wametofautina kutokana na jina hasa la mama huyo. Pia kuna kauli yenye kupingana na usemi wa wanazuoni hawa, kwani baadhi ya wanazuoni wa zama zilizopita na wa zama za hivi sasa, wamenukuu habari mbali mbali kuhusiana na mama huyo, na mmoja ya wao ni Sistani, yeye ameashiria kuwa mama huyo ametokea mji wa Sindiy au Kaabuliy, yeye alielezea hilo kwa kutoa ushahidi kutoka katika vitabu mbali mbali bila ya kutaja mahala alipotekwa binti huyo, bali yeye alimtaja binti huyo kwa jina la Ummu-Walad lenye kumaanisha kuwa yeye alikuwa ni suria aliyezaa mtoto katika hali ya usuria.[11]
Baadhi ya wanatarehe wamemnasibisha mama huyo na baadhi ya watu muhimu wenye hadhi kama vile: Sanjaan, Nushjaan na Shiirwiye, huku wakisema kuwa binti huyo alikuwa ni binti wa mmoja kati ya watu hao maarufu tuliowataja. Kwa kweli si jambo la rahisi kuweza kuipa kipau mbele moja kati ya Riwaya hizo, kwa zote ni zenye utata katika njia za mapokezi yake.
Hivyo basi ni vizuri zaidi kuzichunguza Riwaya hizo kupitia maandiko yake yalivyo. Uchunguzi juu ya maandiko ya Riwaya hizi, unaonesha kuwa Riwaya hizi zote zina aina mbali mbali za utata, na mingoni mashaka makubwa yanayoonekana ndani yake ni kama ifuatavyo:
1- Riwaya zilizomzungumzia binti huyu, hazikuwafikiana kuhusiana na jina hasa la binti huyu, Riwaya hizo zimeonekana kumtaja yeye kwa jina la Share-Baanu huku Riwaya nyengine zikiamini kuwa yeye alikuwa akiitwa Salaakhe, pia kuna Hadithi nyengine zilizosema kuwa yeye alikuwa akiitwa Ghazaala.
2- Kuna utata pia kuhusiana na zama halisi alizotekwa binti huyo, wengine wamesema kuwa alitekwa katika zama za utawala wa Omar, huku wengine wakisema kuwa yeye alitekwa katika zama za utawala wa Othman, pia kuna wengine kama Sheikh Mufiid wanaoamini kuwa yeye alitekwa katika zama utawala wa Imamu Ali (a.s).[12]
3- La msingi pia ni kwamba vitabu muhimu vya Tarehe kama vile Taarekhe Tabariy na Al-Kaamilu-fit-taariikh cha Ibnu Athiir vimenukuu habari za vita baina Waislamu na dola la Wapashia hatua baada ya hatua, huku habari za kukimbia kwa mfalme Yazdgerd wa dola hiyo kutoka mkoa mmoja hadi mwengine, au kitongoji kimoja hadi chengine zikionekana kukoza rangi zaidi ndani ya tokeo hilo, lakini hakukuonekana aina yoyote ile ya ashirio maalumu lenye kuashiria kutekwa kwa binti huyo, iweje basi vitabu hivyo viwe vimelifumbia macho tokeo kubwa na muhimu kama hilo, huku vitabu hivyo vikionekana kunukuu habari mbali mbali hata zile ndogo ndogo zisizo na umuhimu maalumu katika uwanja wa tarehe.
4- Baadhi ya waandishi wa Tarehe waliotangulia kama vile Mas-uudiy, pale walipokuwa wakimzungumzia mfale Yazdgerd wa dola ya Kipashia, walisema kuwa yeye alikuwa na watoto waitwao: Ardak, Shaahin na Mard-aawand, huku katika majina hayo kukiwa hakuonekani lile jina la mama wa Imamu Sajjaad (a.s), pia katika nukuu hizo hakukuonekana habari zinazoonesha kuwepo kwa mwana fulani aliyetekwa katika vita.[13]
Kwa hayo yote tuliyoyasema, sisi hatutoweza kutoa aina maalumu ya kauli kuhusiana na mama wa Imamu Sajaad (a.s), kwani hadi Karne ya tatu kulikuwa kukinukuliwa habari zinazosema kuwa yeye alikuwa ni mkaazi wa Kaabul,[14] hivo basi ni vigumu kutoa kauli ya mkato kuhusiana na suala hilo.[15]
[1] Uyuunil-Akbarir-Ridhaa, juz/2, uk/128, kilichorekebishwa na kufafanuliwa na Sayyidu Mahdiy Huseiniy Laajurdiy, chapa ya mwaka 1377 Hijiria, kilichochapishwa na Mirza Muhammad Ridhaa Muhtadiy.
[2] Muntahal-Aamaal, cha Sheikh Abbaas Qummiy, ju/2, uk/30, chapa ya Hijrat.
[3] Usulil-Kafi, juz/1, uku/467, chapa ya Akhondiy.
[4] Rejea kitabu (Khulasatul-Aqwaal-fi-maa’rifatir-rijaal, sehemu ya pili, uk/241, mlango wa saba, kwenye neno Amru.
[5] Taarikhu Ya’aqubiy, ju/2, uk/303.
[6] Taarekhu Qum, uk/195.
[7] Usuli-Kafi, juz/2, uk/369.
[8] Biharul-Anwaar, juz/46, uk/9.
[9] Uyuni-Akhbaarir-Ridha, juz/2, uk/128.
[10] Al-Irshaad, uk/492.
[11] Biharul-Anwaar, juz/46, uk/9.
[12] Al-Irshaad, uk/492.
[13] Zindeganiy Ali bin Husein (a.s), uk/12.
[14] Shuu’biyya, uk/305.
[15] Rejea Mama wa Imamu Sajjaad (a.s).