Please Wait
14207
Tukitoa jawabu ya kiujumla jamala kuhusiana na swali hilo lililoulizwa hapo juu, tunasema kuwa: si katika zama za zamani au za hivi sasa tu, bali katika zama zote hakujawahi kutokea mtu aliyeweza kuja na maneno yenye kufanana na Qur-ani kiufasaha na kibalagha, bali ufasaha unao onekana ndani ya Qur-ani, ni umahiri pekee usiyoweza kuonekana ndani ya maneno ya mtu yeyote yule wa zama hizi au wa zama zilizokwisha pita zamani, lakini kuna mambo mengine ya kimiujiza yaliyozihusu zama za zaman tui, huku miujiza hiyo ikiwa ni yenye kuhesabiwa kuwa ni jambo la kawaida ndani ya zama za hivi sasa, lakini bado kutabakia mambo mengi yaliyokuwa hayajaweza kupatiwa ufumbuzi wa kielimu hadi leo. Na tusisahau pia, baadhi ya miujiza ya Qur-ani ilikuwa inahusiana na Yule aliyeteremshiwa Qur-ani hiyo, kwani si katika zama zilizopita wala zijazo, hakukutokea mtu zaidi ya Mtume (s.a.w.w) aliyeweza kuja na kitabu kinachofanana na Qur-ani, huku kitabu hichi kikibakia kuwa ni muujiza wa milele uliyowashangaza werevu na wajinga wa jamii mbali mbali, waliyoishi ndani ya zama na mahali tofauti, twasema hayo huku tukiwa na yakini kuwa: hakutatokea mtu awezaye kuja na kitabu kama hichi.
Kinachofuata sasa, ni kuichunguza mitindo mbali mbali ya miujiza ipatikanayo ndani ya Qur-ani, na jinsi ya uwezo kila mmoja kati yake katika kuthibitisha kuwa Qur-ani inatokana na Mola Mtakatifu.
Muujiza unaohusiana na Yule aliyeteremshiwa Qur-ani, ni wenye kutoa thibitisho la kuwa: Qur-ani ni kitabu kitokanacho na Mola Mtakatifu (s.w), jambo ambalo halitoweza kuwa ni dalili ya kuweza kuthibitisha kuwa: maneno ya Qur-ani pia yanatokana na matamshi ya Mola Mtakatifu Mwenyewe.[1]
Yawezekana kukapatikana utata usemao kuwa: jee Mtume hakuwa na uwezo wa kibalagha na kifasaha, kiasi ya kwamba ashindwe kuyajenga maneno ya Qur-ani katika mtindo huu unao onekana ndani ya Qur-ani? Na kama angelifanya hivyo basi pia mjengeko huo bado ungalihesabiwa kuwa ni wenye kutokana na Mola (s.w), tukizingatia kwa makini tutafahamu kuwa swali hili litabakia kuwa ni swali pofu baada ya kulifahamu kwa makini suala la muujiza wa kibalagha na kifasaha uliyopo ndani ya Qur-ani, kwani kuna tofauti baina muujiza unaohusiana na Yule aliyeteremshiwa Qur-ani (s.a.w.w) na ule muujiza unaohusiana na Qur-ani yenyewe. Na hata kama kutatokea mtu atakayesema kuwa: ni sawa kuwa Mtume hakuwa na uwezo wa kuja na maneno yenye mpangilio wa kibalagha kama Qur-ani ilivyo, lakini pia hakuna dalili inayothibitisha kuwa hakutotokea mtu atakayeweza kufanya hivyo, usemi huu pia ni wenye kukubaliana na ule usemi wetu wa kuwa: Qur-ani haikutokana na Mtume (s.a.w.w) na wala si mpinzani mzuri wa kuupinga usemi wetu huu.
Aina nne maarufu za miujiza zinazotajwa na wanazuoni,[2] zaweza tu kuwa ni thibitisho tosha kuwa Qur-ani ni yenye kutokana na Mola Mtakatifu. Ama miujiza ya kimaneno, kibalagha na kiadadi (Kihesabati), ni miujiza tosha ithibitishayo kuwa Qur-ani nzima, yaani maneno pamoja na mtindo wake ni vyenye kutokana na Mola Mtukufu.[3] Pia kupatikana fungamano madhubuti ndani ya Aya zake ni dalili tosha ithibitishayo uhakika huo. Lakini juu ya yote hayo bado tutakabiliwa na swali lisemalo kuwa: jee mfumo wa upangaji wa Aya na Sura za Qur-ani pia unatokana na Mola?
Jawabu ya swali hili unaweza kuipata katika vitabu vinavyozungumzia hali nzima kuhusiana na elimu ya (tarehe ya Qur-ani).[4]
Baadhi ya wanazuoni wa kisunni na wengi miongoni mwa wanazuoni wa Kimagharibi ni wenye kushikamana na mtazamo huo, usemao kuwa Qur-ani iliopo mikononi mwetu imepangiliwa na kupewa mfumo huu tuuonao hivi sasa na masahaba. na haikuwa ni amri itokayo kwa Mola Mtukufu.[5][6]
Kwa utafiti zaidi rejea kitabu: mabani kalaamiy ijtihadi, cha Mahdi Haadawiy Tehraaniy.
[1] Wengine ni wenye mtazamo huo, ingawaje wanaamini kuwa maelezo yake yanatokana na muongozo wa Mola Mtakatifu, lakini wana amini kuwa matamshi ya Qur-ani ni ya Mtume mwenyewe (s.a.w.w). Huku wazazuoni wa Kiisalamu waliopita na wa hivi sasa wakiamini kuwa: tofauti iliyopo baina ya hadithi Qudusiy na Qur-ani ni kwamba: hadithi Qudusiy huwa zinatokana na muongozo wa Mola, huku maneno yake yakiwa ni ya Mtume mwenyewe (s.a.w.w), lakini Qur-ani miongozo na maneno yake yote ni yenye kutokana na Mola Mwenyewe.
[2] Rejea cd ya: namaye katika mada ya miujiza ya Qur-ani.
[3] Yawezekan maulamaa wetu tokea zamani waliutilia mkazo zaidi muujiza wa kibalagha, kwa kutokana na kuwa muujiza huu ni wenye nguvu zaidi katika kuitihibitisha haki.
[4] Kwa mfano unaweza kurejea kitabu: taarekhel- Qur-aan, cha Abdullahi Zanjaniy, pia: taarekhel-Qur-ani cha Muhammad Raamyaar, pazuuhesh dar taarekh Qur-aan, cha Sayyid Muhammad Baaqir Hujjatiy, taarekh jam-e Qur-aan Kariim cha Muhammad Ridha Jalaaliy Naainiy.
[5] Rejea cd ya Namaye: katika mada ya miujiza ya Qur-ani.
[6] Rejea kitabu: mabaani kalaamiy ijtihadi, cha Mahdi Haadawiy Tehraaniy, uk: 52-53, chapa ya kwanza ya Muasaseye farhangiy khaaneye khirad Qum, mwaka 1377 Shamsia.